Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema serikali imejipanga kufikia uchumi wa viwanda, ambao unaendana na kasi ya ukuaji katika sekta ya kilimo hivyo imeweka msukumo mkubwa kwenye mazao yenye thamani kubwa, ikiwemo zao la parachichi. Dk. Mpango amesema hayo katika mkutano wake na wakulima pamoja na wawekezaji wa zao hilo mkoani Mbeya. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angelah Kairuki, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe na vilevile wataalamu na wadau kutoka taasisi mbalimbali.
Waziri huyo ameeleza kuwa, mchango wa kilimo katika kujenga uchumi wa nchi ni mkubwa kwani theluthi mbili ya watanzania wote wanategemea kilimo, hivyo kuinua kilimo cha parachichi kitasaidia kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.
“Parachichi ni zao jipya lakini lina thamani kubwa sana, ulimwenguni linajulikana kama dhahabu ya kijani. Ili kuzalisha kwa wingi zao hili wakulima wetu hasa wadogo wadogo wanatakiwa wawe na mitaji, utaalamu, sehemu ya kuhifadhia mazao yao na kuwepo na masoko ya kuuzia zao hilo, hasa masoko ya nje ambayo yataingizia nchi fedha za kigeni”. Amesema Waziri Mpango.