Watanzania wametakiwa kutumia ukubwa wa soko la Afrika Mashariki kujiinua kiuchumi kupitia bidhaa zilizoboreshwa za kilimo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji),Dk. Doroth Mwaluko kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa saba wa kitaifa wa utafiti wa uunganishaji wa mifumo ya kuinua uchakataji wa bidhaa za kilimo (7th NRG) uliofanyika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii-ESRF.
Katika hotuba yake hiyo kwenye Mkutano; huo uliokuwa unazungumzia mnyororo wa thamani katika kilimo kwa Afrika Mashariki,iliyosomwa na Ezamo Maponde kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maendeleo ya Sekta Binafsi alisema ukubwa wa soko unaleta maana zaidi kama mifumo itaoanisha kuwezesha ukuaji wa soko na huduma zake.
Alisema katika mkutano huo kwamba Afrika Mashariki ina jumla ya wananchi milioni 172 huku asilimia 22 ya wananchi wake wakiishi katika miji.
Aidha alisema takwimu zinaonesha kwamba nchi hizo zina pato la taifa za dola za Marekani bilioni 172 kufikia Desemba 2017, linatosha kukuza mnyororo wa thamani wa bidhaa za kilimo.
Alisema katika mkutano huo unaozungumzia utafiti kuhusu maendeleo endelevu ya mchakato wa kuongeza mnyororo wa thamani Afrika Mashariki na kuimarisha mahusiano ya kinchi, kwamba kuna changamoto nyingi zinazokumbwa juhudi hizo na lazima zitafutiwe tiba.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni tamaduni na namna ya kizamani ya kuchakata bidhaa, kuingizwa kwa bidhaa zilizochakatwa kutoka ughaibuni, uzalishaji mdogo wa wakulima unaotokana na matumizi hafifu ya pembejeo, ukosefu wa taarifa za masoko na bei ya bidhaa zisizo na tija.
Dk Mwaluko alisema kwamba mkutano huo una maana kubwa kwa kuwa unasaidia kuianisha mambo, kuyatambua na kuyatafutia suluhu ili kutekeleza Azimio la Malabo la kuongeza tija katika kilimo na pia matumizi ya soko la ndani kuinua kilimo.
Alisema kwa sasa taifa kama la Tanzania lenye uzalishaji mkubwa wa mahindi, muhogo, viazi mbatata, viazi vitamu, ndizi, mtama na sukari halina sababu ya kuwa na wakulima maskini kwa kuwa soko lipo.
Alisema ili kuweza kufanikiwa ni vyema kuunganisha nguvu katika jumuiya kuondoa vikwazo na kuiweka sekta ya uchakataji imara kwa kuwezesha maendeleo ya kilimo na uchumi wa mataifa ya Afrika Mashariki.
Dk Mwaluko alisema mkutano huo ambao unafanyika kipindi cha pili cha uboreshaji wa kilimo wakati wa mabadiliko ya tabia nchi, wataalamu wanatakiwa kujikita kukabili changamoto zilizopo ili kuikuza sekta ya kilimo na kuwezesha viwanda vinavyotegemea mazao ya kilimo kukua.
Alisema kukosekana kwa taratibu mtambuka kunachochea changamoto zilizopo katika kilimo na hivyo ipo haja ya kuangalia sera na kushawsihi mabadiliko ili kukiidhi mahitaji ya sasa.
Alitaka katika maamuzi pia kutosahau nafasi ya kibiashara ya kimataifa katika ukuzaji wa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania.
Mkutano huo ulioendeshwa na ESRF kwa ushirikiano na taasisi ya CUTS International ya Geneva ulijadili mada mbili zinazohusu uwekaji wa maunganiko katika mifumo inayoinua sekta ya kilimo na uchakataji wa bidhaa.
Akimkaribisha Mwakilishi wa Dk Mwaluko kuzungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida alisema kwamba mkutano huo ni matokeo ya tafiti zinazofanyika kuhusu maendeleo ya kilimo.
Alisema kwamba hakuna maunganiko ya moja kwa moja katika sera na sheria zinazogusa kilimo cha uchumi na kusema ipo haja ya wataalamu kuangalia na kushawishi masuala mtambuka ya kilimo kuangaliwa kwa pamoja.