Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba ametoa wito kwa waandaaji wa maonyesho ya Nanenane kuhakikisha kuanzia mwakani, maonyesho hayo yanapewa sura mpya itakayoleta mabadiliko kwa wakulima, wafugaji pamoja na wavuvi na kuwapatia uwezo wa kuzalisha kwa tija.
Dk. Tizeba amesema hayo wakati akihutubia wananchi katika Uwanja wa Nanenane uliopo Nyakabindi Bariadi na kuongeza kuwa, waandaaji wanapaswa kuhakikisha maonyesho hayo yanawafundisha wananchi na yanatumika kama darasa huru la kubadilishana uzoefu ili kuleta matokeo mazuri katika sekta ya kilimo.
“Kuanzia Nanenane ya mwaka huu na zinazofuata, waandaaji naombeni mzipe sura mpya na hata tunapowaomba wadau kuchangia maandalizi wawe wanaamini kuwa tutakachokifanya kitaleta mabadiliko chanya kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii”. Amesema Waziri huyo.
Akizungumzia maonyesho hayo, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa maonyesho ya nanenane Nyakabindi ili kupata nafasi ya kujifunza masuala mbalimbali kwani waonyeshaji wa teknolojia mbalimbali wanapatikana mahali hapo.