Kila mkulima huwa na ndoto ya kupata mazao mengi na kufanya biashara ili kupata faida. Nyanja ya muhimu katika kila biashara ni soko. Inashauriwa kufanya uwekezaji wa kutosha katika upande masoko ili kutangaza bidhaa na kupata wateja wengi zaidi. Kama mkulima unayetaka mafanikio, unajua baadhi ya mambo ya kufanya ili kupata masoko ya uhakika?
Haya ni baadhi ya mambo muhimu ambayo mkulima anatakiwa kufanya ili kupata masoko ya uhakika.
Tambua wateja wako
Wakulima wengi wamejiwekea kuwa wanaweza kuuza kwa mtu yoyote. Hiyo inaweza kuwa kweli kwa kiasi fulani, lakini kama mkulima makini mwenye malengo ya kufanikiwa kupitia kilimo ni vyema kujua bidhaa zako zinalenga wateja wa aina gani. Kwa mfano unaweza kujiuliza je, bidhaa unazouza hununuliwa zaidi na wanawake au wanaume? Je, wateja wako wengi ni vijana, wazee? Wateja wako wengi ni watu wa kipato gani? Unapofahamu wateja wako, inakurahisishia kutengeneza bidhaa zako katika mtindo sahihi.
Kuwa tofauti
Hapa mkulima anatakiwa kujiuliza kwanini mteja aje kununua bidhaa kwangu? Kwa maana nyingine katika biashara yako kuna vitu gani vya kipekee ambavyo mteja anaweza kupata? Unaweza kujitofautisha na washindani wako kwa kuuza mazao yanayotoka moja kwa moja shambani (fresh), au unaweza kujikita kwenye kuuza mazao yenye ubora wa hali ya juu, au kuwa na huduma nzuri kwa wateja.
Jitangaze
Maisha yamebadilika sana siku hizi na teknolojia zinaendelea kuboreshwa ili kurahisisha mawasiliano baina ya watu. Hivyo basi, kama mkulima mwenye malengo ya kufika mbali unatakiwa kuwa na jina au utambulisho ambao utakusaidia kujitangaza. Aidha, unaweza kuanzisha tovuti inayoelezea kazi yako kwa ufupi ikiwa ni pamoja na aina ya mazao unayolima na bidhaa zinazopatikana. Unaweza kuweka bei za bidhaa zako na mawasiliano ili wateja waweze kukufikia kwa urahisi. Kilimo cha kisasa kinatakiwa kwenda kisasa ili kupata mafanikio zaidi.
Jiunge na vikundi, hudhuria mikutano
Kwa kujiunga na vikundi wakulima wanakuwa na uhakika wa kujipatia masoko ndio maana serikali imekuwa ikiwasisitiza kujiunga na vikundi mbalimbali ili kuweza kupata elimu, mafunzo na masoko. Pia kupitia vikundi ni rahisi kutengeneza mtandao na kupata taarifa kuhusu mambo mbalimbali kuhusu kilimo jambo ambalo ni muhimu kwa mkulima. Mbali na kujifunza, unakuwa unajitangaza na kutokana na mtandao huo, unapata nafasi ya kukua kibiashara.
Mbali na hayo, mkulima anatakiwa kuzingatia ubora wa huduma inayotolewa kwa wateja wake ili kuweza kupata mafanikio. Ikiwa umeajiri wafanyakazi hakikisha nao wanahudhuria semina na mikutano ya kilimo ili waweze kufanya kazi zao ipasavyo.