Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amewaonya wafanyabiashara wanaouza mbegu pamoja na viuatilifu feki, na kusema hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Hasunga ameeleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika, Prof. Shaukat Abdulrazak na kuongeza kuwa, Tanzania ni moja kati ya mataifa ambayo kumekuwa na changamoto kubwa ya wananchi kuuziwa mbegu feki.
Katika maelezo yake, Waziri huyo amesema Wizara ya Kilimo imekuwa mstari wa mbele kuboresha kilimo kwa kutumia teknolojia lakini uwepo wa viuatilifu feki sokoni umekuwa ukirudisha nyuma jitihada kubwa zinazofanywa na wakulima.
“Wananchi wetu wanajitahidi kulima kwa kiasi kikubwa, lakini kumekuwepo na changamoto kubwa ya viuatilifu na mbegu feki. Jambo hili hatuwezi kuliacha na hivi karibuni nimetangaza kiama na wafanyabiashara wanaosambaza kuwa tutakapowabaini tutawachukulia hatua kali sana”. Amesisitiza Hasunga.
Kwa upande wake, Prof. Abdulrazak amesema mkutano wake na Waziri Hasunga umeimarisha ushirikiano ambao amedai umekuwepo kwa kipindi kirefu na Shirika hilo.