Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema filamu ya “The Royal Tour” imefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kwamba kwa sasa watalii wameongezeka.
Masanja ameyasema hayo alipotembelea maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba.
Filamu hiyo, ilizinduliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunatambua kwamba ni nadra sana kumpata kiongozi anayeamua kuongoza kwa vitendo kama alivyofanya Rais Samia, ametangaza kwa vitendo vivutio vyetu hivyo tunatakiwa kuvitembelea ili kumuunga mkono,” amesisitiza Masanja.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwahimiza Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko nchini akitolea mfano wa maeneo ya Malikale, Misitu ya Asili, tamaduni za Kitanzania, historia za Tanzania za Waasisi wa Taifa na maeneo mengine ya utalii.
“Tutembelee vivutio vyetu, ukishakitembelea kile kivutio unakuwa umechangia pato la Taifa lakini hata wewe mwenyewe utakuwa umejifunza historia ya nchi ilivyo lakini pia utapunguza hata msongo wa mawazo,” amesema Masanja.