Home MAHOJIANO Hongera Rais Samia

Hongera Rais Samia

0 comment 125 views

Leo Januari 27, 2022 ni kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Watu mbalimbali, taasisi zilizo za serikali na za binafsi wamemtakia kheri Rais Samia. Ama kwa hakika salamu katika siku yake hii muhimu sio haba.

Rais Samia leo ametimiza umri wa miaka 62, amesema yeye ni mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto 15 lakini mama wawili. Baba yake akiwa ni mwalimu na mama zake wawili wakiwa ni mama wa nyumbani wakifanya biashara ndogo ndogo.

Akieleza kuhusu makuzi yake pamoja na elimu Rais anasema “niseme kwamba kuanzia darasa la awali mpaka nimefika kidato cha nne nimesoma shule kama kumi hivi, na hiyo ni kwasababu baba yangu alikuwa mwalimu, kwahiyo alikuwa anahamishwa vituo vingi vingi vya kazi, kwahiyo kila akihamishwa na mimi nipo nyuma.

Nikiwa na miaka minane tisa ivi niliishi na dada yangu ambae yeye alikuwa ni muuguzi na wakati ule walikuwa wanapangwa vijijini na alikuwa peke yake akasema ngoja niende na mdogo wangu kwahiyo nikaanza kuishi nayeye kwa miaka kadhaa. Kutoka hapo mpaka nimekuwa mkubwa nilikuwa mikononi kwake, kwa hiyo nimezunguka kiasi Fulani. Ukienda kwenye visiwa vya Zanzibar Unguja na Pemba mimi ni mwenyeji sana.”

Kwa sasa Rais Samia ana Shahada ya Uzamili (Masters Degree), anasema “nilijaribu labda kufanya PhD ukweli ni kwamba pilika ni nyingi na nimeshindwa, sijui niseme nimeshindwa au ntaimalizia baadae sijui labda ntaimalizia baadae.”

Akielezea maisha yake ya kazi, Rais ameeleza kuwa alifanya kazi serikalini kwa miaka kadhaa na baada ya hapo alifanya kazi na mashirika mengine mbalimbali ya kimataifa kabla ya kurudi serikalini.

Kuhusu siasa amesema mwaka 2000 ndio alipata mawazo ya kuingia kwenye siasa.

Leo Rais samia pia alieleza anachofanya anapokuwa amechoshwa na majukumu na kusema

“ukiona kichwa kimejaa zaidi tiba yangu ni wajukuu, napiga tuu simu nileteeni hao, wanakuja pale kwa masaa kadhaa hasa nikiwa Dar es Salaam, kwa masaa kadhaa piga kelele panda shuka pigishwa mbio kwenye ngazi wakirudi wanapokaa basi ubongo umepumzika.

Taarabu kidogoo, eeeh hio ndo sana, hata nikiwa nadeal na mafaili apo pembeni icho kitu kipo, kazi na dawa.”

Katika kusheherekea siku hii muhimu amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii.

“Tutakaoijenga hii nchi ni sisi Watanzania na tutakaoibomoa ni sisi Watanzania, nchi haijengwi na mtu mmoja, inajengwa na kila mmoja wetu kwenye mchango wake,” amesema Rais Samia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter