Baada ya Samsung kusitisha uzinduzi wa simu mpya ya Samsung Galaxy Fold mwezi Aprili mwaka huu kufuatia malalamiko kutoka kwa watumiaji wa majaribio, kampuni hiyo inategemea kuzindua rasmi simu hiyo mwezi huu ambapo kwa kuanza itazinduliwa South Korea 07/09/2019, na kuna tetesi kuwa itazunduliwa nchini Marekani 27/09/2019.
Sifa zake:
Samsung Galaxy Fold ni zaidi ya simu janja, ni kifaa kinachoweza kukunjwa na kubadilika kutoka katika muonekano wa simu kwenda kwenye muonekano wa kompyuta kibao (Tablet) na kurudi tena. Ikiwa imefungwa, Galaxy Fold ina sentimita 6.3 kwa upana na sentimita 16 kwa urefu (2,5 kwa inchi 6.3) na ikiwa imefunguliwa kikamilifu, ina urefu wa inchi 7.3 ambayo ni sawa na (sentimita 18.5). Simu hii inavunja rekodi kwa kuwa simu kubwa zaidi kutengenezwa na Samsung.
Simu hii ni nzuri ikiwa unataka kwa picha na video, kusoma barua pepe, michezo nk. Samsung hii ina uwezo wa kutumia/kufungua hadi programu tatu kwa wakati mmoja. Pamoja na hayo, Galaxy Fold ina kamera sita ambapo katika kamera ya nyuma, kuna lensi tatu kama ilivyo katika simu ya Samsung galaxy s10+, (12MP Wide Angle Camera, 12MP Telephoto camera, 16MP Ultra wide). Lensi nyingine iko kwenye kifuniko karibu na screen ya pili huku lensi mbili zikiwa katika kamera ya mbele (10MP x 2 selfie cameras, 8MP RGG depth camera) . Pia kuna skana ya alama ya vidole katika upande wa kulia na inaweza kutumika wakati wowote (simu ikiwa wazi au ikiwa imezimwa).
Kwa upande wa betri, imegawanywa katika pande mbili za simu kwa ndani. Pia, simu hii ina uwezo wa kuchaji wireless earphones, saa za Galaxy na hata simu nyingine bila kutumia waya (Wireless). Hadi sasa Samsung haijatoa makadirio kamili ya uwezo wake wa kukaa na chaji lakini inaelezwa kuwa inategemea matumizi ya mtu.
Simu hiyo inatarajiwa kuingia sokoni kwa gharama ya Dola za kimarekani 1,980, ambayo ni takribani milioni 4 za kitanzania. Galaxy fold ina processor ya kisasa ya Snapdragon-855 na RAM ya GB 12. Kuhusu uhifadhi wa taarifa katika simu hiyo, mtumiaji ana uwezo wa kuhifadhi data hadi za 512 GB, ambazo ni nyingi lakini ni chache ikilinganishwa na simu ya Samsung Galaxy S10+ ambayo ina uwezo wa kuhifadhi data hadi za TB 1. Mfumo wa mtandao utakaotumika katika simu hiyo, hadi sasa kuna uhakika wa mfumo wa 4G. Uwezo wake wa mfumo wa 5G unategemewa kuwekwa wazi baada ya uzinduzi rasmi.