Na Mwandishi wetu
Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo imejenga kisima cha maji chenye thamani ya Sh.18 milioni katika kijiji cha Usongelani wilayani Urambo mkoa wa Tabora. Katika sherehe ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Tigo kanda ya ziwa Ally Maswanya amesema kisima hicho kitasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa maji kwa wananchi wa eneo hilo.
Maswanya ameongeza kuwa Kampuni ya Tigo inajitahidi kuboresha maisha ya jamii sio tu katika huduma za mawasiliano bali katika masuala ya afya na ustawi wa wananchi. Msaada huo utanufaisha wananchi zaidi ya 187,000 huku mkurugenzi huyo akidai kampuni hiyo inalenga kuchimba vizima zaidi katika maeneo yaliyo na uhitaji mkubwa.
Katika sherehe hizo pia, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameshukuru kampuni ya Tigo kwa msaada wa kujenga kisima hicho akisema kitasaidia kuimarisha afya kwa kiasi kikubwa na pia kusaidia ukuaji wa wananchi kiuchumi na kijamii.