Tume ya Madini imesema katika mwaka wa fedha wa 2024-2025 inakusudia kukusanya maduhuli kiasi cha shilingi trilioni 1.
Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo Ramadhan Lwama, amesema hayo jijini Dar es Salaam, Oktoba 24, 2024 katika Kikao Kazi baina ya Tume na Wahariri na Waandishi wa Hbaari, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kikao hicho kimelenga kueleza mafanikio ya tume katika kipindi cha miaka 3 ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kinachotupa matumaini kufikia trilioni 1 ni mikakati tuliyojiwekea kufika maeneo ambayo hapo awali hatukuweza kufika, kuhamasisha wachimbaji kuongeza uzalishaji lakini pia kuhakikisha usalama unazingatiwa ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa uzalishaji na uuzaji wa bidhaa za madini,” ameeleza Lwama.
Amesema kupitia wataalamu wa tume, wamekuwa wakiwahamasisha wachimbaji kufanya uchimbaji kwa tija, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha timu za kudhibiti utoroshaji wa madini zinafanya kazi yake ipasavyo.
Ili kuthubitisha kufikiwa kwa lengo hilo la makusanyo, Lwama amesema katika robo ya kwanza pekee, tayari tume hiyo imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 257.89.
Lwamo amesema kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini, kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu.
“Mathalan katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo tulipewa lengo la kukusanya shilingi Trilioni Moja, hadi kufikia Oktoba 21, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 312.75 sawa na asilimia 31.28 ya lengo la mwaka,”amesema Mhandisi Lwamo.
Amesema, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023 hiyo ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini nchini.
Mhandisi Lwamo amesema vilevile, ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023 kutokana na kuendelea kuimarika kwa Sekta, Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa utaongezeka na kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoelezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Alex Malanga, Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina, amesema ni dhamira ya Ofisi ya Msajili kuona taasisi za umma, zinaweka utaratibu wa kukutana na wahariri ili kueleza nini ambacho taasisi hizo zinafanya.
Akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Mjumbe wa tume hiyo, Jane Mihani ameishukuru ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuweka utaratibu ambao umekuwa ukisaidia wanachi kupitia vyombo vya habari kujua serikali inafanya nini.