Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) anayeshughulikia masuala ya kodi za ndani, Michael Muhoja amesema takribani wamachinga 20,000 kote nchini wanatarajiwa kusajiliwa na TRA baada ya mamlaka hiyo kuzindua usajili wa wafanyabiashara wadogo kupitia vikundi vyao kwa lengo la kuwatambua na kurasimisha shughuli wanazofanya.
Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere amezungumzia usajili huo na kufafanua kuwa ni utekelezaji wa sheria ya bunge inayohusu kutambulika kwa wafanyabishara wadogo ili waweze kushiriki katika ujenzi wa taifa kupitia kodi na ushuru mbalimbali kama ambavyo sheria inaelekeza.
Katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Mwanza, Mkuu wa mkoa huo, John Mongella alitoa agizo kwa halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wafanyabiashara ambao wamesajiliwa na TRA wanapata mikopo ya asilimia 10 kupitia vikundi vyao.