Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho amesema Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linatarajia kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Zambia, Zimbabwe na China kupitia Thailand huku vituo vitano vya ndani ya nchi vikiongezwa. Dk. Chamuriho amesema hayo wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya Airbus A220-300 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es salaam.
Katibu huyo amefafanua kuwa huo ni utekelezaji wa awamu ya pili ya upanuzi wa mtandao wa ATCL baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza. Vituo vya ndani vitakavyoongezwa ni pamoja na Mpanda, Pemba, Iringa, Kahama, Musoma. Aidha, safari za kuelekea Songea na Mtwara nazo zinatarajiwa kurudishwa.
“Utekelezaji wa safari hizo za ndani utatokana na kukamilika kwa utekelezaji wa ujenzi wa viwanja hivyo juu ya ujenzi wa miundombinu unaofanyika pamoja na uwepo wa abiria wa kutosha ikiwamo mbinu za kibiashara”. Amesema Dk. Chamuriho.
Mbali na hayo, Dk. Chamuriho amesema uwezo wa ndege za ATCL katika kubeba abiria umeongezeka na kufikia 34,000 kwa mwezi huku umiliki wa soko la ndani ukiongezeka hadi asilimia 31 kufikia Oktoba mwaka huu. Vilevile, Katibu huyo amesema ATCL imepiga hatua kwa kuruka kwa ndege na kutua kwa wakati kutoka asilimia 22, Oktoba 2016 hadi kufikia asilimia 80 mwaka huu.
“Tunalipa kodi serikalini, tunawekeza katika ukodishaji pesa, hizi zote ni faida ambazo zinapatikana katika uendeshaji wa shirika hili. Tunaendelea kutumia bidhaa zinazozalishwa na kuchakatwa ndani ya nchi”. Amesema Dk. Chamuriho