Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe amesema hadi kufikia Julai mwaka huu, bandari kavu iliyopo Kwala mkoani Pwani itakuwa imekamilika na kuanza kutumika.
Waziri Kamwelwe ameeleza hayo baada ya kuzindua bandari kavu yenye uwezo wa kuhifadhi magari 1,000 ya Kitopeni jijini Dar es salaam. Waziri huyo ameeleza kuwa mizigo inayotoka bandari ya Dar es salaam itaelekezwa katika bandari hiyo ili kupunguza adha ya msongamano.
“Kuna changamoto nyingi kwa wanaosafirisha mizigo kwenda Kongo kupitia mpaka wa Kasumbaleza, ni hatari, magari yana foleni zaidi ya kilomita 70, tatizo hili nalijua baada ya Bunge nitakwenda kuonana na Waziri mwenzangu huko Zambia kuona uwezekano wa kujenga njia nyingine ambayo ni fupi. Kwa kuwa hapa kitopeni pamekamilika kazi kwenu TRA, magari yakiingia bandarini yaje huku yasisongamane na kontena kwani ni hatari. Kuanzia leo magari yakifika yaje huku, TRA mkajipange mje huku kwa ajili ya kodi”. Amesema Waziri huyo.
Naye, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam, Fredy Liundi, amesema bandari hiyo inaendelea kupokea mizigo ya ndani na nje ya nchi na eneo la Kitopeni limeendelezwa ili kukidhi mahitaji ya mizigo hiyo.