Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja amewasihi wananchi wa Mkuranga na maeneo jirani vumilia kero ya maji ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na kuwahakikishia kuwa ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, watapata maji ya uhakika.
Mhandisi Luhemeja amesema hayo akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji katika eneo hilo na kueleza kuwa, DAWASA imetumia fedha za ndani takribani Sh. 5.6 bilioni kuanza mchakato wa kupeleka mabomba na kuyalaza kuanzia ulipo mradi na kuyapeleka maeneo ya karibu ya Mkuranga. Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji inatarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu.
“Mkandarasi ataingia kazini mwezi Mei mwaka huu, na kuanzia kesho tutafanya kazi ya ulazaji mabomba yatakayokuwa na urefu wa kilomita 15″. Amesema Mhandisi Luhemeja.
Afisa huyo amesema hadi sasa ni wananchi 2,500 pekee kati ya 25,500 ndiyo wanapata huduma ya maji na kuongeza kuwa wamechimba kisima cha urefu wa mita 600. Mbali na hayo, DAWASA pia inajipanga kujenga tanki ambalo litahifadhi lita 1.5 milioni kwa siku.
“Tayari uchimbaji wa kisima chenye urefu wa mita 600 umekamilika”. Amesema Mhandisi Luhemeja.