Kiongozi wa Mwenge 2019, Mkongea Ali, amekataa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa zaidi ya Sh. 800 bilioni wa Itumba Isongole mkoani Mbeya baada ya kubaini kwamba nyaraka ya taarifa na ile inayoelezea ujenzi zinatofautiana. Kiongozi huyo amedai imeshindikana kuweka jiwe la msingi katika mradi huo ambao unategemea kuwanufaisha wananchi zaidi ya 3000 kutokana na upungufu huo kwani kwa taratibu zilizopo, lazima nyaraka maalum ambayo inaonyesha gharama zilizoongezeka kwenye mradi iandaliwe kwa sababu fedha zinazotumika ni za serikali.
“Mshauri wa mradi ni mtu muhimu sana sasa kwanini hayupo hapa wakati yeye ndiye mwakilishi wa serikali, nani atatupa maelekezo yanayoeleweka kama yeye hajajua umuhimu wake na umuhimu wa mbio za mwenge kwenye miradi ya serikali, pia kwanini msimamizi aliruhusu gharama kuongezeka kwenye mradi huu bila maelekezo au nyaraka yoyote inayoonyesha gharama kuongezeka”. Amehoji Kiongozi huyo
Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude kufuatilia suala hilo kwa kina akishirikiana na vyombo husika ili kujua ukweli wa mabadiliko hayo. Kwa Upande wake, Mhandisi wa mradi huo, Abdallah Digelo, amebainisha kuwa mradi huo umechelewa kutokana na mabadiliko na maboresho waliyoyafanya kwenye tanki pamoja na usafi wa miundombinu katika eneo hilo.