Home VIWANDAMIUNDOMBINU Bila maji, uchumi wa viwanda ni ndoto

Bila maji, uchumi wa viwanda ni ndoto

0 comment 65 views

Tanzania imeipokea kwa mikono miwili dhana ya kubadilisha nchi yetu kuwa ya uchumi wa viwanda. Mpaka hivi sasa kumekuwa na mabadiliko mbalimbali katika sekta ya viwanda ambayo serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wamependekeza ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za viwanda vya hapa nchini. Moja kati ya changamoto kubwa katika kuboresha viwanda hapa nchini ni upatikanaji wa maji. Ukweli ni kwamba viwanda haviwezi kusonga mbele bila uwepo wa maji ya uhakika. Sekta ya viwanda inategemea maji ili kufanikisha shughuli zake na kusaidia ukuaji wa uchumi. Hivyo basi ni muhimu kujiuliza, miundombinu ya maji iliyopo hivi sasa inaendana na kasi ya uboreshwaji wa viwanda?

Tayari serikali imeweka wazi kuwa imedhamiria kubadilisha uchumi na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Ni ukweli kuwa nchi haiwezi kuendelea bila sekta ya viwanda. Lakini tumejipangaje kuboresha viwanda vya hapa nchini? Wizara ya maji imejipangaje kuhakikisha kuwa maji sio tena changamoto kwa viwanda na hata matumizi ya kawaida ya nyumbani? Huwezi kufanya kazi vizuri kama unaumwa kutokana na kunywa maji yasiyo salama hivyo athari za maji huanza moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida mpaka kufikia ngazi za kimaendeleo kama viwanda.

Ili kufanikisha lengo la kufikia uchumi wa kati mwaka 2025 suala la maji halipaswi kuachwa nyuma. Wadau wa masuala ya maji wanatakiwa kushirikishwa kikamilifu ili serikali ifikie azma hii ya uchumi wa viwanda. Viwanda haviwezi kuendelea kuzalisha bidhaa bila maji. Hivyo ili kukuza uchumi kwa kasi kwa kupitia sekta hii ni lazima kuwe na mpango madhubuti ili kukabiliana na changamoto za maji zilizopo.

Awali katika Bunge la Bajeti 2017/2018 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Gerson Lwenge alisema sekta ya maji hapa nchini inakumbwa na changamoto mbalimbali na mojawapo kati ya hizo ni kupungua kwa rasilimali hiyo kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kote nchini. Mabadiliko ya tabianchi na matumizi mabaya ya maji pia ni changamoto kubwa katika sekta hii.

Hivyo basi ili kufikia lengo la uchumi wa viwanda, ni muhimu kwa serikali pamoja na watanzania kwa ujumla kusimamia rasilimali za maji na kuhakikisha kuwa hakuna uharibifu unaoendelea ili kusaidia rasilimali hizo ziendelee kuwepo. Kama ambavyo wadau wa maendeleo walivyopokea hili la viwanda basi wanatakiwa pia kuhakikisha kuwa miundombinu yote ya maji inatunzwa na kutumika inavyotakiwa kwani bila ya kuwa na matumizi sahihi ya maji na kutunza vyake, Tanzania ya viwanda itabaki kuwa ndoto tu.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter