Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kutoka Mradi wa mabasi yaendayo kasi (Udart) Deus Bugaywa amewaambia waandishi wa habari kuwa mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es salaam zimepelekea mabasi 29 yaendayo kasi kuharibika kutokana na eneo lao la maegesho kukumbwa na mafuriko na kujaa maji.
Mabasi hayo ambayo huegeshwa eneo la Jangwani ambalo hivi sasa limejaa maji na kusababisha shughuli zinazoendeshwa na mradi huo kusitishwa kwa muda ili kutafuta eneo lingine la kufanyia kazi. Maji kutoka Mto Msimbazi yamekuwa yakiingia kwa kasi katika eneo la maegesho ya magari hayo kutokana na ukuta kubomoka.
Mbali na athari hizo, kampuni hiyo imelazimika kuwapa likizo wafanyakazi wake mpaka pale eneo jipya la kufanyia kazi litakapopatikana.