Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema uzinduzi wa Minara ya mawasiliano ya simu kwa kiasi kikubwa itaiwezesha Zanzibar kuingia katika Teknolojia ya Mawasiliano ya TEHAMA.
Amesema hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi pamoja na kukua kwa sekta ya Uwezeshaji kiuchumi.
Dkt. Mwinyi amesema hayo katika Ufunguzi wa minara 42 pamoja na vituo 11 vya TEHAMA huko Bwefuu, Mkoa Mjini Magharibi, iliyojengwa kupitia fedha za ruzuku za mfuko wa mawasiliano kwa wote.
Alisema, matumizi ya huduma za mawasiliano kwa sasa hayaepukiki kwa sababu mawasiliano yanagusa moja kwa moja maisha ya wananchi, ikiwemo walioko vijijini katika shughuli zao za kila siku.
Akitolea Mfano, Dkt. Mwinyi amesema matumizi ya TEHAMA yamekuwa yakiongezeka ikiwemo maeneo ya vijijini na kuchukua fursa kubwa za kiuchumi na hivyo kuongeza kipato cha wananchi.
Amesema “nachukua nafasi hii kuupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwa kushirikiana na Kampuni za Tigo/Zantel katika ujenzi wa Minara 42 na Vituo 11 vya TEHAMA hatua inayokwenda kufungua fursa muhimu za Uwekezaji na kiuchumi.”
Aidha, Dkt. Mwinyi aliwataka wakazi wa maeneo hayo kuitunza miundombinu hiyo na kuepuka uharibifu unaoweza kurudisha nyuma hatua kubwa ya maendeleo iliofikiwa.
Dkt. Khalid Salum Mohammed, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji amesema uzinduzi wa minara hiyo ni sehemu ya ahadi ya kufikisha mawasiliano vijini na kuondosha kabisa tofauti iliopo kati ya maeneo ya miji na vijiji.
“Kinachofanyika leo ni kufikisha huduma za maendeleo kwa kasi kubwa na huduma za mawasiliano hadi vijijini ili kuondoa tofauti na pengo la huduma hizo”, amesema.