Kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024, serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wa bwawa la Yongoma lililopo Wilayani Same.
Lengo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuinua kipato cha wakulima.
Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde amesema hayo wakati wa ziara ya kikazi wilayani humo kukagua maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji na miundombinu yake.
“Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaendelea kukipa kilimo kipaumbele cha juu, ambapo bajeti ya mwaka 2023/2024 ametutengea fedha kiasi cha bilioni 970, kati ya fedha hizo zaidi ya bilioni 384 zimeelekezwa kwenye umwagiliaji”
“Msukumo huo mkubwa kwenye kilimo unaooneshwa na Rais wetu ndo unapelekea Tume yetu ya Taifa ya Umwagiliaji kuendelea na ujenzi wa skimu, visima na mabwawa nchi nzima ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao nchini”, amesisitiza. Mavunde.
Ameeleza kuwa kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 serikali imepanga kujenga miundombinu mbalimbali ya umwagiliaji vikiwemo visima 150 kwa kila Halmashauri, mabwawa 100 nchi nzima ambayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji ya umwagiliaji takribani lita za ujazo bilioni 900.
Hii ni kumwezesha mkulima kuzalisha mwaka mzima pasipo kutegemea mvua na hatimaye kuongeza tija ya uzalishaji na kipato cha kaya na Taifa kwa ujumla.
Awali, akieleza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Same Mashariki, mbunge wa jambo hilo Anne Kilango-Malecela ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyoendelea kuwakumbuka wananchi wake.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amebainisha kuwa pamoja na upembuzi yakinifu, usanifu na ujenzi wa bwawa la Yongoma, serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/24 pia itafanya ukarabati wa mifereji ya skimu ya Ndungu ambayo inatoa maji mto Yongoma ili kuhakikisha wakulima wanufaika wapatao 3000 wanazalisha kwa tija kwenye hekta 680 za skimu.