Home VIWANDAMIUNDOMBINU TIC yasema kukamilika kwa uwanja wa ndege jengo la tatu kutavutia wawekezaji wengi zaidi

TIC yasema kukamilika kwa uwanja wa ndege jengo la tatu kutavutia wawekezaji wengi zaidi

0 comment 121 views

Na Grace Semfuko-MAELEZO.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kinatambua kuwa miezi michache ijayo serikali kwa kukamilisha ujenzi wa majengo na ufungaji wa mitambo ya kisasa kukidhi mahitaji ya teknolojia ya kimataifa, jengo la tatu (Terminal 3)  Uwanja wa Kimataifa Julius Nyerere( JNIA) ni ukurasa mpya wa fursa za kuongeza kasi ya  uwekezaji hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TIC, Geoffrey Mwambe alitembelea eneo la ujenzi na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania ( TAA), Richard Mayongela kwa ziara ya kutambua zaidi mapya ya jengo la tatu ili kumpa nafasi ya kujenga vishawishi kwa wawekezaji kuhusu manufaa ya chombo hicho kinachokamilika wakati tayari tatizo la foleni ya magari toka uwanjani huo kuingia jijini umeisha  baada ya barabara la juu kukamilika katika maungo ya barabara za Mandela toka bandarini na Nyerere itokayo JNIA.

TIC ni taasisi ya serikali, imekuwa ikifanya juhudi za kufafanua kwa wawekezaji fursa zilizopo Tanzania kwa lengo la kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje  nchi , na hivyo kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo na kuwa chombo chenye kila hitaji la abiria wa anga katika dunia ya sasa, utaongeza idadi ya wawekezaji  kwa sababu ya huduma mpya hizo. “Huduma yetu usafiri wa anga inabadilika kabisa” amesema Mkurugenzi Mkuu TAA, Mayongela.

Mayongela amesema kukamilika kwa uwanja huo mpya jengo la tatu kutaondoa kabisa msongamano wa abiria uliopo uwanja wa pili (Terminal 2) uliojengwa miaka 34 iliyopita, ambao kwa wakati huo ulilenga kuhudumia abiria Milioni 1.5 na sasa umezidiwa kwa kuhudumia abiria hadi milioni   2.5 kwa mwaka,  kutokana na ongezeko la abiria nahatimaye kusababisha kuzidiwa kwa uwanja huo.

Uamuzi wa kujenga kituo cha pili (Terminal 2) ulioazimiwa na serikali mwaka 1984 ulitokana na kuwepo kwa ongezeko la abiria kituo la kwanza (Terminal 1) kilichojengwa mwaka 1956, ambapo kituo kilikuwa na uwezo wa kuhudumia abiria laki tano tu, hatua iliyosababisha Serikali kujenga uwanja huo wa pili ambao nao kwa sasa umelemewa na abiria wengi.

“Ujenzi wa uwanja huu ni mkombozi mkubwa kwetu watanzania katika kuboresha sekta ya anga,uwanja wa ndege tunaoutumia sasa ulijengwa mwaka 1984 ,ni miaka 34 mpaka sasa kwa hiyo utaona ni jinsi gani tulivyo bize kuhudumia abiria kwa idadi iliyolengwa mwaka huo kwa sasa watu tumeongezeka na hivyo serikali imefanya jambo la msingi sana kujenga uwanja huu” Alisema Mkurugenzi Mkuu TAA.

Hata hivyo, vituo viwili vilivyopo, uwanja huo JNIA bado vilikuwa na mapungufu ya mahitaji ya kisasa kwa dunia inayobadilika kila siku kiteknolojia, na Mkurugenzi Mkuu wa TIC ameelezwa huduma sasa zitakuwa na viwango vya kuhudumia kila aina ya makundi ya watu maarufu na kituo sasa kitaweza kupokea aina yoyote ya ndege pasipo kuhofia ubora ama ukubwa wake.

Kadhalika,  naye Bw. Mwambe amekiri na kufurahishwa na hatua za uboreshaji wa usafiri wa anga uliofikiwa na taifa na kuongeza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutasaidia kuongezeka kwa tija kwenye uwekezaji, kwani abiria na mizigo ya wawekezaji itahudumiwa kwa usafiri wa anga.

“Usafiri wa anga una uhusiano mkubwa na kuimarisha uwekezaji nchini,wawekezaji wengi wanaingia nchini kupitia usafiri wa anga,wanakuja na kuleta vifaa vya uwekezaji kwa kutumia usafiri wa aina mbalimbali ukiwepo usafiri huu wa anga,kwa hiyo kukamilika kwa uwanja huu kutatusaidia sisi kuimarisha sekta ya uwekezaji Nchini na ndio maana nimekuja kuangalia maendeleo yake” Alisema Bw.Geoffrey Mwambe Mkurugenzi Mtendaji wa TIC.

“Abiria wa kigeni akitua Tanzania kitu cha kwanza atakachokutana nacho ni sura ya nchi ambayo inatambulishwa na uwanja wa ndege mzuri, sisi Tanzania tupo vizuri! Napenda kuishukuru serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli kwa kuimarisha miundombinu, tumeona hivi karibuni Rais akizindua barabara ya juu ya Mfugale,tunaona kasi ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge, ujenzi wa uwanja huu na mengineyo mengi,kwetu sisi TIC tumefarijika kwani wawekezaji sasa watapata urahisi wa usafirishaji” Alisema Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC.

Jengo hilo jipya la tatu la uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere,  litahusika na  ndege za kimataifa tu na litahudumia abiria milioni 6 kwa mwaka, na kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria hata 2,800 kwa saa kwa wanaoingia na kutoka,  na pia utahudumia ndege kubwa 19 na ndege ndogo 11 zinazoingia na kutoka nchini  kwa wakati mmoja.

Ujenzi wa Jengo la tatu (Terminal 3) JNIA ulioanza Juni, 2013 na utakaogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 560 unakabidhiwa rasmi mamlaka husika tayari kwa kuutumia Mei, 2019 ukiwa katika viwango vyote vya kimataifa na kwa sasa wajenzi wanasema kazi ilyosalia ni ndogo ya asilimia 17.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter