Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba ya mkopo yenye masharti nafuu ya dola za Marekani milioni 161.47 na euro milioni 110, mtawalia, sawa na shilingi 647.5bn.
Mkopo huo utawanufaisha wakazi wa Mkoa wa Kagera kuondokana na changamoto ya kukosa umeme wa uhakika.
Mikataba imesainiwa na Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini Tanzania Dkt. Patricia Laverley na Bi. Celine Robert, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa.
Waziri Dkt. Nchemba amefafanua kuwa kati ya fedha hizo zilizosainiwa, kiasi cha dola milioni 161.47 sawa na shilingi bilioni 374.9 kimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB na kiasi cha euro milioni 110 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 272.6 kimetolewa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa-AFD.
“Katika kutatua changamoto za nishati ya umeme mkoani Kagera, Serikali iliiomba AfDB na AFD kufadhili Mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono, ambapo kwa pamoja – AfDB; AFD kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Tanzania zimekubali kufadhili mradi huu wenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 325 sawa na shilingi 750 bilioni,” amesema Dkt. Nchemba.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imeshuhudiwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa nchi na mashirika ya kimataifa, akiwemo Naibu Balozi wa Ufaransa Axel Guillon. Mkuu wa Ushirikiano wa EU nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Cedric Merel na ujumbe kutoka Mradi wa Umeme Kakono na TANESCO.