Home VIWANDANISHATI Manufaa ya gesi asilia Tanzania

Manufaa ya gesi asilia Tanzania

0 comment 131 views

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaeleza kuwa gesi asilia ni mchanganyiko wa molekuli nyepesi nyepesi za carbon na Hydrogen mfano: Methane (CH4), Ethane (C2H6). Gesi hii inatokana na kuoza kwa mata organia (organic matter) kama vile uozo wa masalia ya mimea na wanyama miaka mingi iliyopita. Gesi asilia inapatikana kwenye mwamba wenye vinyweleo vingi ulioko chini ya ganda la mwamba imara zaidi unaozuia gesi kupanda juu zaidi.

Kwa hapa Tanzania, Shirika hilo linajihusisha na utafutaji, uchimbaji, uendelezaji pamoja na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kusambaza gesi au mafuta kwa wateja.

Hadi kufikia sasa, gesi asilia imeanza kuvunwa kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara. Imeanza kusambaza katika maeneo hayo kwa mfano kwa wananchi wa kawaida na kwenye viwanda kama kiwanda cha saruji kilichopo Mtwara kinachomilikiwa na Dangote. Vilevile gesi hiyo inatumika kuzalisha umeme nchini na baadhi ya wakazi wa jijini Dar es salaam wameanza kunufaika na gesi asilia baada ya kufanyika majaribio Mikocheni na kupata matokeo mazuri.

Gesi asilia inategemewa kuuzwa kwa bei nafuu zaidi kuliko gesi ya mitungi (Liquidfied Petroleum Gas) ambayo imekuwa ikiagizwa kutoka nje jambo ambalo limesababisha bei zake kuwa juu kidogo hivyo si kila mtanzania anaweza kumudu bei hizo.

Faida za Gesi Asilia:

  • Gesi asilia ni salama zaidi kuliko gesi ya kwenye mitungi, mafuta, mkaa, kuni hasa majumbani kwa sababu gesi hiyo ni nyepesi zaidi kuliko hewa hivyo itakapotokea gesi hiyo imevuja kwa bahati mbaya itapaa na kupotea kwa haraka zaidi.
  • Gesi asilia ni bei rahisi zaidi kwa sababu inazalishwa nchini kuliko gesi ya mitungi ambayo hutolewa nje ya nchi.
  • Matumizi ya gesi asilia ni mkombozi wa misitu na mazingira hivyo majanga kama mmomonyoko wa udongo, uharibifu na ukame yatapungua endapo wananchi watahamia kwenye matumizi ya gesi.
  • Pia gesi asilia ni salama kwa afya ya watumiaji kwa kuwa haina moshi na haitoi harufu.
  • Kwa matumizi ya gesi asilia kwenye vyombo vya moto, mtumiaji hutumia nishati hiyo kwa kiwango kidogo kuliko akitumia mafuta kwa sababu gesi huisha taratibu zaidi.

Hasara za Gesi Asilia:

  • Hadi sasa, wananchi ambao wameanza kunufaika na gesi hiyo wametoa malalamiko kwamba gesi wanayosambaziwa ni ndogo hivyo kusababisha hasara katika biashara zao zinazohitaji nishati hiyo.
  • Bado uzalishaji wa nishati hiyo ni ndogo na mahitaji ya wananchi ni makubwa.
  • Kwa sababu haina harufu, ni rahisi kusambaa sehemu kubwa bila mtumiaji kugundua hivyo ni rahisi kulipuka na kusababisha maafa ya moto. Ingefaa kama watumaji wote wakipewa elimu ya kutosha ili kuepukana na athari hiyo, na kuwepo na watu maalumu ambao watakuwa wakikagua mara kwa mara kwa watumiaji na kuendelea kuwaelimisha.

Kwa ujumla, utafiti unathibitisha kwamba gesi asilia ni nzuri zaidi kuliko nishati nyingine kwa asilimia 90%. Hivyo uzalishaji zaidi, ujenzi wa miundombinu mathubuti pamoja na elimu ni muhimu ili kuwasaidia watanzania kutumia gharama ndogo kwenye matumizi yao ya nishati ya kila siku.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter