Home BIASHARA Ongezeko kodi ya majengo kuanza kesho

Ongezeko kodi ya majengo kuanza kesho

0 comment 38 views

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza ongezeko la kodi ya majengo kupitia manunuzi ya luku kuanzia kesho Ijumaa Agosti 20, 2021.

Kwa ongezeko hilo, kwa sasa wenye nyumba za kawaida ndani ya kiwanja kimoja watalipa Sh12, 000 kutoka Sh10, 000 iliyokuwa ikitozwa awali na Sh60, 000 kwa kila sakafu ya ghorofa kutoka Sh50, 000.

Kwa upande wa Halmashauri za Wilaya na Miji Midogo wao watalipa Sh60, 000 kwa nyumba za ghorofa bila kujali idadi ya sakafu

Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Alphayo Kidata leo inaeleza kuwa utekelezaji huo unafanyika chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ukihusisha mita za aina zote za umeme.

Taarifa hiyo inasema “hili linafanyika kufuatia marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sura ya 289 iliyopitishwa na Bunge la Bajeti la mwaka 2021 ambapo viwango vya kodi ya majengo vimebadilishwa.”

Inaeleza kuwa njia hii mpya ya ukusanyaji wa kodi, kila mnunuzi wa umeme atakatwa Sh1,000 kwa mwezi kwa nyumba ya kawaida na Sh5,000 kwa mwezi kwa kila sakafu ya ghorofa.

“Kwa wale wanaotumia mita za Ankara watalipa kodi hii kwa pamoja katika Ankara ya mwezi. Kwa wamiliki ambao majengo yao hayajapata umeme, wataendelea kulipa kodi hiyo kwa kutumia mfumo uliokuwa unatumika hapo awali ambao ni njia ya simu ya mkononi na benki baada ya kupata namba ya kulipia malipo (Control Number) mpaka hapo watakapoingiziwa umeme,”

Kodi ya Majengo ilikuwa ikikusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo mwaka 2016/17 jukumu hili lilihamishiwa TRA.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter