Mawaziri kutoka Tanzania, Burundi na Rwanda wanaosimamia utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Rusumo (MW 80) wamekagua kazi ya ujenzi wa mradi huo mkoani Kagera na kutoa maelekezo mbalimbali yatakayochochea kasi ya mradi huo kuongezeka. Katika ukaguzi huo, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amewaongoza Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi, Come Manirakiza na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Claver Gatete.
Baada ya ukaguzi huo, Mawaziri hao walifanya kikao na kuiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya mradi huo kusimamia kazi mbalimbali za ujenzi ili zikamilike hadi kufikia mwaka 2020. Kwa mujibu wa Dk. Kalemani, kazi ya ujenzi wa mradi huo ilianza mwezi Februari mwaka 2017 na inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36.
“Pia tumeiagiza Bodi na wataalam walioko katika mradi huu, wahakikishe kuwa wanashirikisha mamlaka na taasisi mbalimbali zilizopo katika maeneo ya mradi katika nchi zote tatu hasa katika masuala yanayohusu jamii zinazozunguka mradi na stahili za wafanyakazi ili kutokuwa na vikwazo katika utekelezaji”. Amesema Dk. Kalemani.
Tanzania, Rwanda na Burundi zote zimegharamia mradi huo kupitia Benki ya Maendeleo Afrika (AfdB) na Benki ya Dunia (WB) ambapo kwa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme, kila nchi imechangia Dola za Marekani 113 milioni.