Home VIWANDANISHATI Nishati isiyo safi inavyogharimu maisha ya Watanzania elfu 33 kwa mwaka

Nishati isiyo safi inavyogharimu maisha ya Watanzania elfu 33 kwa mwaka

0 comment 64 views

Zaidi ya watu elfu 33 wanakufa kila mwaka nchini Tanzania kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na nishati isiyo safi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo Septemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Hafla ya Azimio la Kizimkazi iliyolenga kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya Kupikia.

Ametoa wito kwa Watanzania kuokoa maisha yao kwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ambayo itawaepusha na madhara yanayotokana na nishati isiyo safi ikiwemo athari katika mfumo wa upumuaji pamoja na vifo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akimkabidhi mmoja wa baba lishe jiko la gesi.

“Kwa bahati mbaya ya nishati isiyo safi, madhara yake hayawezi kuonekana leo, wala huwezi kuyaona kesho, nilikuwa mahali nikawambia madhara ya nishati isiyo safi huwezi kufananisha na kipindupindu wala corona ama ugonjwa mwingine wa mlipuko unaoua mara moja. Unamuua mtu polepole,” ameeleza Dkt. Biteko.

Akitoa takwimu za hali ilivyo kwa sasa, Dkt. Biteko amesema watu bilioni 5.8 duniani ndio wanatumia Nishati Safi huku Bilioni 2.4 wakitumia Nishati isiyo safi ambapo Afrika pekee ina watu milioni 933 wanaotumia nishati isiyo safi na hivyo kuwataka wadau kuuganisha nguvu kuunga mkono matumizi ya nishati iliyo safi.

“Nipende kumpongeza sana Rais kwa kuibeba ajenda hii ya Nishati safi ya Kupikia na kwa maono aliyonayo, nitoe agizo kwa watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha Wizara inashirikisha wadau kwenye kampeni hii ili iweze kufanyika kwa ufanisi na hivyo kumuunga mkono Rais,” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesema, Rais Samia licha ya kuwa kinara wa Afrika kwenye kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, pia amedhamiria kuwaondoa kina mama na baba lishe wa Tanzania katika matumizi ya nishati isiyo safi na pia kuboresha hali zao kwa kutumia nishati safi ya kupiki ambapo ametoa mitungi 2,000 kwa kundi hilo kama njia ya uhamasishaji wa nishati hiyo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter