Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Njombe, Yusuph Salim amewataka mafundi umeme katika mkoa huo kupata leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ili kupunguza matatizo wanayokumbana nayo wateja kutoka kwa watoa huduma za umeme wasio rasmi, maarufu kama vishoka.
Kaimu huyo ametoa wito huo wakati akizungumza na mafundi umeme na wahandisi mkoa wa Njombe katika mkutano wa pamoja ulioandaliwa na umoja wa makandarasi (UMAU).
“Fundi yeyote kwa sasa mkoani Njombe anatakiwa awe na leseni ya Ewura na hii kupata ni muda mfupi sana tena kwa gharama ndogo ya elfu 60 tu, sidhani kama kuna fundi atashindwa hili, kigezo cha kwanza mtu anapokwenda kufanya kazi katika nyumba yeyote awe na leseni, wateja wetu niwaombe tusifanye kazi na watu wasiokuwa na vigezo ili hata ikitokea matatizo aweze kushtakiwa na kunyang’anywa leseni pamoja na kuchukuliwa hatua nyingine”. Amesema Salim.
Aidha, Kaimu huyo amewaonya wakandarasi wenye mazoea ya kuwaongopea wananchi, hasa wale wanaoishi vijijini kuwa wanafanya kama TANESCO na watafikisha huduma ya nishati ya umeme.