Kufuatia maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama mahali pa kazi yaliyofanyika jijini Mbeya, Meneja Masoko wa Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mussa Chowo amesema shirika hilo limesamehe riba kwa wateja wake na kuwataka kulipa fedha kamili wanazodaiwa.
Meneja huyo amesema msamaha umeanza rasmi jana (Mei Mosi), lengo likiwa ni kuwezesha shirika hilo kupata Sh. bilioni 300 ambazo wanadaiwa wateja.
“Shirika la TANESCO limeamua kutoa msamaha kwa wateja wake baada ya malimbikizo makubwa ya madeni yaliyopo na wadeni makubwa ni kutoka katika ofisi za serikali na wananchi, lengo letu ni kurejesha fedha tunazowadai ambazo ni Sh. bilioni 300 tunawasisitiza kulipa kwa wakati”. Amesema Chowo.
Pamoja na hayo, amewasisitiza wananchi kuendelea kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati hiyo kwa ajili ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Naye Ofisa Afya na Usalama wa shirika hilo, Nelson Mnyanyi amesema licha ya kutoa elimu na ushauri kwa wazazi kuhusu umakini kwa watoto katika maeneo yao, shirika hilo pia limejipanga kutoa elimu mashuleni na katika taasisi nyingine ili kukabiliana na majanga yanayotokana na umeme.