Kaimu Mkurugenzi wa mkondo wa chini kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert amesema Shirika hilo lina mpango wa kuwahamasisha watanzania wote kutumia nishati ya gesi hadi kufikia Mei 2020. Gilbert amesema kuwa zoezi la usambazaji wa gesi jijini Dar es Salaam linaendelea kutokana na bajeti iliyopo ambapo inatarajiwa kuwa, takribani Dola za Marekani 270 milioni (Sh. 623 Bilioni) zitatumika.
Hadi sasa gesi hiyo ambayo inasemekana kuwa na ujazo wa futi trilioni 57.54 imekuwa ikitumika kwa matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya uzalishaji wa umeme. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ikiwa inategemea gesi kwa asilimia hamsini.
“Kabla ya kutumia gesi hii nilikuwa nanunua mkaa gunia moja kati ya Shilingi 60,000 hadi 80,000 ambalo halikutosha hata kwa matumizi ya mwezi mmoja”. Amesema Angela Joseph, mkazi wa Dar es salaam ambaye kwa sasa anafurahia matumizi ya gesi.
Ofisa Utafiti wa TPDC, Eva Swillah amesema Tanzania ina gesi ya kutosha na matumizi ya gesi ni salama na nafuu, na kwamba miundombinu ndiyo inakwamisha usambazaji wa gesi nchini.