Meneja Mradi Matumizi katika kuleta Maendeleo, Fredrick Tunutu amesema wajasiriamali 349 kutoka katika vijiji 59 vya mikoa ya Tanga na Pwani wamenufaika na mradi wa matumizi mazuri ya nishati kwa kufanya shuguli za kimaendeleo ikiwemo kufungua biashara ndogo ndogo. Tunutu amesema hayo kwenye kikao cha kujadili mipango na bajeti ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) wakati akitoa tathmini ya mradi wa huo unaodhaminiwa na Norway.
Katika maelezo yake, Meneja huyo ameeleza kuwa wajasiriamali wote waliosajiliwa wamepewa washauri ili wajue mambo ya kuzingatia ili kukuza biashara zao. Kupitia ushauri huo, wamefanikiwa kupata faida kwa asilimia 87 ikiwa ni kutoka dola za Marekani 43,000 wakati mradi unaanza mwaka 2018 hadi dola 81,000 kufikia Machi mwaka huu.
“Takwimu zilizokusanywa mwishoni mwa utekelezaji wa miradi hiyo zilionyesha kwamba faida ya jumla waliosaidia biashara hizo imeongezeka kwa asilimia 87″. Amesema.
Kuhusu mikopo, Tunutu wafanyabiashara waliokidhi vigezo vya kupata mikopo wameweza kukuza mapato yao kwa asilimia 46, huku wale ambao hawakukidhi wakiwa wamekuza mapato yao kwa asilimia 26.
Biashara zilizosaidiwa kupitia mradi huo zimeweza kuongeza ajira kwa asilimia 46 huku watu 214 wakiajiriwa ajira za kudumu na utoaji wa mikopo hiyo rasmi imetolewa kwa watu 121 kwa muda wa miezi tisa na 274 mikopo isiyo rasmi.
“Mikopo hiyo imetumiwa kupata vifaa na kuboresha uwezo wa uendeshaji wa baadhi ya biashara. Mpango huo pia umewezesha ugavi wa vifaa vingine 339 vilivyochangia ongezeko la nishati ya umeme kwa asilimia 80 katika kipindi cha miezi tisa kutoka wastani wa 42kWh kwa mjasiriamali mmoja julai mwaka jana na kufika 75kWh ilipofika Machi mwaka huu”. Ameeleza Tunutu.
Aidha, Meneja huyo ametaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni muitikio mdogo wa taasisi za kifedha katika utoaji mikopo kwa wafanyabiashara na riba kubwa inayosababisha marejesho ya mikopo hiyo kuwa mahivyo kuwa tatizo.