Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesisitiza kuwa ufungaji wa mgodi wa Buzwagi hautaathiri shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Kahama, kwani mipango madhubuti imewekwa kuhakikisha kuwa eneo hilo linaendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kupitia miradi mipya ya uwekezaji na maendeleo.
Amesema hayo Februari 16, 2025 Kahama Mkoani Shinyanga wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyotembelea eneo la Mgodi wa Buzwagi ambao uko kwenye hatua za kufungwa baada ya kusitisha uzalishaji wa madini ya dhahabu.
Dkt. Kiruswa alibainisha kuwa, mradi wowote unapoanzishwa lazima mwekezaji aonyeshe mpango wa ufungaji mgodi kabla ya kukabidhiwa leseni na kuendeleza maeneo husika ambako moja ya masharti ni pamoja namna ya kuendeleza shughuli za kiuchumi katika jamii zinazozunguka mradi bila kuathiri maendeleo endelevu ya kiuchumi na mzunguko wa fedha.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ng’enda alieleza jinsi Kamati ilivyovutiwa na mchakato huo wa ufungaji Mgodi wa Buzwagi.
Ng’enda alisisitiza kuwa, maelekezo ya Bunge ni kuhakikisha eneo hilo linabaki kuwa mfano wa uwekezaji wa viwanda hapa nchini kwa manufaa ya kiuchumi kwa jamii na taifa.
Naye Meneja wa Ufungaji Mgodi wa Barrick Buzwagi, Zonnastral Mumbi, amesema Barrick itaendelea kushirikiana na Serikali wakati wote kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vya kimataifa na kuwa mfano wa kuigwa kwa kufunga shughuli za mgodi na kuacha eneo lililokuwa mgodi linakuwa na miradi endelevu ya kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa, nia ya Kampuni ya Barrick ni kuhakikisha kuwa inaacha urithi mzuri ambao utaendelea kuhudumia jamii kwa muda mrefu baada ya uchimbaji kufikia mwisho katika mgodi huo, kupitia miradi ya kilimo, ufugaji wa kuku na nyuki, chuo cha ufundi na miundombinu mengine ya maji, barabara na uwanja wa ndege wa Kahama.