Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Charles Mwijage ametoa wito kwa wakulima wa mihogo kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao hilo badala ya kuangalia bei iliyopo kwa wakati huo. Mwijage amewataka wakulima kufanya hivyo licha ya serikali kutambua kuwa bei ya bidhaa hiyo haijapanda kulingana na kilimo chenyewe akieleza kuwa ni mkakati mojawapo wa kuboresha soko la zao hilo nchini.
“Uzalishaji unapaswa kuongezeka kwa usawa na usawa halisi ni tani 30 kwa hekta na si vinginevyo. Wafundisheni wakulima wajitahidi kuzalisha kwa kiwango hicho”. Ameeleza Mwijage.
Mbali na kilimo cha mihogo, Waziri huyo amewataka wakulima wa miwa kuongeza uzalishaji na kuzingatia ubora. Vilevile, Mwijage ametoa wito kwa wazalishaji wa mbegu ya mpunga yenye harufu ya Aroma kuzingatia ubora na kuongeza zaidi uzalishaji wao ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi zinapokuwa sokoni kutokana na mbegu hizo kutopatikana kwa urahisi ikilinganishwa na mbegu nyingine.
Kwa upande wake, Mtafiti wa Kilimo ambaye pia ni Ofisa Mfawidhi wa TARI Dakawa, Dk. Charles Chuwa amesema uchache wa mbegu hizo sokoni unatokana na uzalishaji mdogo huku akibainisha kuwa wakulima wengi huvutiwa zaidi kutumia mbegu aina ya TXD 360-Saro 5 ambayo huzalisha takribani tani sita hadi nane kwa hekta.