Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imejipanga kuwekeza katika rasilimali watu na fedha ili kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda.
Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Tamko la Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu uwekezaji huo lililotolewa jijini Dar Es Salaam mwezi Julai 2023.
Hayo yamebainishwa jijini Luanda, Angola na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax kwenye Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioshirikisha nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.
Dkt. Tax amesema tamko la Dar Es Salaam limeainisha masuala mbalimbali ya utekelezaji kwa ajili ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu ambayo yameendelea kujadiliwa katika Mkutano wa 43 wa SADC.
Amesema wanataka kuhakikisha kuwa, katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inahusu umuhimu wa rasilimali watu na fedha katika maendeleo endelevu ya viwanda, tamko la Dar Es Salaam linakuwa sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu hiyo.
“Suala la uwekezaji katika rasilimali watu, suala la uendelezaji wa rasilimali watu katika kuendeleza uchumi, ni vitu ambavyo tunaendelea kuvisukuma kama ilivyokuwa kwenye mkutano jijini Dar es Salaam ambapo Rais wetu alikuwa Mwenyekiti wa mkutano ulioangazia masuala ya rasilimali watu uliofanyika Tanzania”, ameeleza Dkt. Tax.
Awali wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Bw. Elias Magosi alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma kasi ya muingiliano, uendelezaji wa viwanda na upatikanaji wa masoko lakini pia nje ya nchi hizo.
Amebainisha kuwa uondoaji wa vikwazo hivyo, utaifanya kanda ya SADC kuwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda wa 2020-2030 na dira ya kanda hiyo ya 2050.