Home VIWANDAUZALISHAJI Taasisi za uhifadhi zatakiwa kulinda maeneo kwa teknolojia

Taasisi za uhifadhi zatakiwa kulinda maeneo kwa teknolojia

0 comments 9 views

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zinazojishughulisha na masuala ya uhifadhi kuhakikisha zinaweka mikakati ya kulinda maeneo ya hifadhi kwa teknolojia.

Ameyasema hayo Machi 29,2025 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Arusha wakati wa ziara ya kikazi ambapo alikagua mradi wa Barabara ya kiwango cha changarawe (km 16) inayogharimu shilingi milioni 417.8 inayounganisha kata ya Ngarenanyuki na Usariva Wilaya ya Arumeru, Mkoani humo.

“Katika kukabiliana na ujangili na uvamizi katika maeneo ya hifadhi, wakati umefika wa kulinda maeneo yetu kwa kutumia teknolojia kama ndege nyuki ‘drones’, darubini, cctv cameras n.k” amesisitiza Balozi Dkt. Chana.

Aidha, ameipongeza menejimenti hiyo kwa utendaji kazi wake na ongezeko la mapato kutoka shilingi bilioni 6 mwaka 2019/2020 mpaka shilingi bilioni 9 mwaka 2023/ 2024 na ongezeko la watalii kutoka 57,697 hadi 81,761 kwa kipindi hicho.

“Nawapongeza na  Rais anafurahishwa na shughuli za utalii zinazoendelea za ukusanyaji wa mapato” amesema.

Katika hatua nyingine, amesisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na mipango ya kuzuia na kupunguza takwimu za majeruhi ya wananchi kutokana na wanyamapori wakali.

Naye Kamishna Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Kuji ameahidi kutekeleza maelekezo yote na kuhakikisha anaboresha zaidi miundombinu ya hifadhi hiyo na kuongeza mapato zaidi.

Balozi Dkt. Chana yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!