Serikali imesitisha uagizaji wa mchele nje ya nchi baada ya kujiridhisha na upatikanaji wa kutosha wa nafaka hiyo. Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mathew Mtigumwe katika mafunzo ya kilimo yaliyowakutanisha wakulima mbalimbali nchini, hafla iliyofanyika mjini Moshi chini ya ufadhili wa Shirika la misaada Japan (JICA). Mtigumwe amesema kuwa uzalishaji wa zao hilo umeongezeka ambapo mpaka sasa kuna tani milioni 1.2 huku mahitaji kwa mwaka yakiwa ni tani 900,000.
“Serikali mwaka huu haina haja ya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi”. Amesema Mtigumwe.
Akizungumzia kuhusu shirika la JICA,, Mtigumwe amesema serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na shirika hilo katika kuinua sekta ya kilimo kwa kuwasaida wakulima wadogo na kuongeza kuwa uzalishaji katika kilimo umekuwa ukiongezeka ikilinganishwa na siku za nyuma.
Akitoa takwimu za ongezeko la uzalishaji wa mpunga, Mtigumwe amedai Tanzania imekuwa ikiongeza juhudi za uzalishaji ambapo mpaka sasa inashika nafasi ya tano katika nchi za ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara ambazo ni Nigeria, Madagascar, Mali na Guinea.
Kwa upande wake, Mkuu wa JICA nchini Toshio Nagase amesema kuwa mpaka sasa, shirika hilo limefanikiwa kusaidia wakulima takribani 15,000 nchi nzima.