Home VIWANDAUZALISHAJI Tathmini yaonesha uwepo wa madini katika eneo la hekari 7,180 mkoani Rukwa

Tathmini yaonesha uwepo wa madini katika eneo la hekari 7,180 mkoani Rukwa

0 comment 123 views

Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo mkoani Rukwa, kutokana na uwepo wa Madini ya Ulanga, Shaba, Emerald, Titanium, Dhahabu, Hellium, Makaa ya Mawe na Aquamarine ili kuvutia wawekezaji na kuongeza tija katika uchumi wa mkoa huo.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema hayo Oktoba 23, 2024, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo ambako amesisitiza kwamba lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zilizopo nchini ikiwemo mkoa wa Rukwa zinawanufaisha Watanzania, ikiwa ni pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza wakati wa ziara ya kikazi Rukwa.

Akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini baada ya kukagua shuguli za uchimbaji mdogo katika kijiji cha Mponda, Manispaa ya Sumbawanga, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa serikali haitaki kuona wachimbaji wadogo wakichimba kwa kubahatisha katika shughuli zao hivyo kupitia Mpango wa Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri Serikali imepanga kuongeza utafiti wa kijiolojia ili kusaidia kuboresha kanzidata ya hifadhi ya madini yaliyopo nchini.

“Ndugu zangu, kiwango cha utafiti wa kina wa kijiolojia kwa Tanzania nzima ni asilimia 16 tu, lakini serikali inalenga kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo na wawekezaji wakiwemo wa Rukwa wanakuwa na taarifa za kina za kijiolojia ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika uchimbaji wa madini kwa kufanya shughuli zao kwa uhakika” amesema Dkt. Kiruswa

Pamoja na hayo, Dkt. Kiruswa amebainisha kwamba Serikali kupitia Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) itaendelea kutoa msaada wa vifaa vya kisasa kwa wachimbaji wadogo, ikiwa ni pamoja na mashine za uchorongaji na kwamba vifaa hivyo vya kisasa vitawawezesha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, kuboresha uzalishaji, na kuongeza thamani ya madini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter