Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati, Mathew Kiondo amesema uzalishaji wa mazao ya nyuki kwenye mashamba ya serikali katika mikoa ya Dodoma ya Singida unatarajiwa kuongezeka maradufu ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kiondo ameeleza kuwa hapo awali mavuno ya mazao hayo yalikuwa ndoo 10 hadi 20 lakini mwaka huu, wanatarajia kupata hadi tani tisa za asali. Meneja huyo ameeleza kuwa mabadiliko yametokana na mapinduzi yaliyofanywa kwenye sekta ya ufugaji nyuki ambapo wameimarisha zaidi usimamazi wa makundi ya nyuki.
“Mwaka huu hasa kituo cha Manyoni tunatarajia kupata tani sita hadi saba na kituo cha Kondoa tunaweza kupata tani mbili”. Amesema.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa wa Wafugaji Nyuki Tanzania (TAPEDO) Rodia Issa ametaja baadhi ya changamoto ambazo wadau wa mazao ya nyuki wanakumbana nazo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa vifungashio na gharama kubwa ya motambo kwa ajili ya uchakataji wa mazao hayo.
Mashamba hayo yamekuwa na manufaa kwa wananchi ikiwemo kuleta fursa mbalimbali za ajira na vilevile kutoa elimu ya utengenezaji mizinga ya kisasa.