Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dk. Edwin Mhede ametoa wito kwa wazalishaji wa muhogo hapa nchini kuzalisha zao hilo kitaalamu, kwa ubora na viwango vinavyohitajika sokoni. Dk. Mhede amesema hayo jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa zao la muhogo uliofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
“Wengi mnafahamu kuwa changamoto katika zao hili ni upatikanaji wa mbegu bora, aina ya mbegu inayoweza kukabiliana na magonjwa mbalimbali mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha uhaba wa upatikanaji wa mavuno ya kutosha na uzalishaji mdogo unaochagizwa na kilimo cha mashamba madogo madogo”. Amesema Katibu huyo.
Katika maelezo yake, Dk. Mhede amesema muhogo ni zao rasmi la biashara hivyo na linachangia kikamilifu katika kuongezea pato la taifa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kwa mwaka 2015/16 zao hilo lilichangia asilimia 13.63 ya pato la taifa. Kati ya mwaka 2012 na 2016, tani 59,447,754 za muhogo ziliuzwa nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa TanTrade, Edwin Rutageruka amesema lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto zinazolikabili zao la muhogo na kuzitafutia ufumbuzi.