Home VIWANDAUZALISHAJI  Waziri Mkuu ataka bidhaa zinazozalishwa nchini kukidhi viwango

 Waziri Mkuu ataka bidhaa zinazozalishwa nchini kukidhi viwango

0 comments 40 views

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi za kudhibiti viwango nchini zihakikishe uzalishaji wa bidhaa  zote zinazozalishwa zikiwemo za afya zinakidhi ubora unaotakiwa na kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa.

Ametoa agizo hilo Machi 20, 2025 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mitambo ya kuzalisha oksijeni kwa matumizi ya hospitali, ambapo amesisitiza kuwa soko linatakiwa liwe na bidhaa salama, bora, na zinazokubalika kimataifa.

Mitambo hiyo inajengwa katika ofisi za TOL Gases, Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema mradi huo utakapokamilika utazalisha lita milioni 4.1 za oksijeni ya matibabu kwa mwaka kuanzia mwaka 2026.

“Hatua hii itaboresha upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na vituo vya afya, pamoja na kupunguza gharama za oksijeni ya matibabu kwa asilimia 35 katika hospitali na vituo vya afya kote nchini, hivyo kuimarisha huduma za afya kwa wananchi”.

Aidha, Waziri Mkuu amesema mradi huu unaunga mkono juhudi endelevu za Serikali za kuhakikisha oksijeni kwa ajili ya matibabu inapatikana kwa urahisi katika kila vituo cha huduma za afya nchini.

“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na zahanati nchini na kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya kupumua ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wa Taifa hili.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godfrey Mollel amesema mradi huo ni muhimu kwa sababu oksijeni inayozalishwa kwa njia hiyo inakuwa na viwango vya ubora, hivyo itasaidia kuimarisha huduma za afya zitolewazo nchini pamoja na kupunguza vifo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases, Daniel Warungu ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujidhatiti katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Amesema kampuni ya TOL inajivunia kushirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya kuboresha huduma za afya, hususani upatikanaji na usambazaji wa gesi ya oksijeni kwa ajili ya matibabu ukiwemo mradi wa shilingi bilioni 9.8 wa ufungaji wa mifumo ya usambazaji gesi wodini katika vituo 129 vya huduma za afya nchini kote.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!