Na Mwandishi wetu.
Baada ya Rais John Magufuli kuonyesha kukerwa na kitendo cha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage kuchelewa kuwanyang’anya umiliki wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda hivyo kwa zaidi ya miaka 20, waziri huyo amesema kuwa hadi kufikia alhamisi wiki hii atakua na orodha kamili ya makampuni yote yatakayochukuliwa hatua hiyo na atayaweka wazi.
Makatibu wakuu wa wizara zote zinazohusika na viwanda watashirikiana na wakuu wa mikoa yote nchini kuzungumzia suala hili. Waziri Mwijage amechukua hatua hiyo kwasababu viwanda vingine vipo chini ya wizara tofauti hivyo anawajibika kusikia kutoka kwao.
Tangu kuingia madarakani serikali ya awamu ya tano imekua mstari wa mbele kuwasihi watanzania kuanzisha na kuwekeza katika viwanda. Wananchi walioitikia wito huu wamekua wakikumbana na changamoto kadhaa kama gharama za kununua maeneo na kuboresha miundombinu. Kuwapa watanzania umiliki wa viwanda hivi kutasaidia kupunguza adha hizi na hivyo kuviendeleza.
Hatua ya serikali kumilikisha upya viwanda hivi ni tumaini jipya kwa watanzania kujipatia maendeleo. Tanzania hii mpya ya viwanda itazalisha ajira kwa wazawa na pia kuwa fursa nzuri ya wakulima kupata soko la mazao yao hivyo kuimarisha uchumi wetu.