Benki ya Access Tanzania Limited kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), wametoa mafunzo ya msingi ya ujasiriamali kwa wafanyabiashara wanawake jijini Dar es salaam na kuanzisha akaunti ya “Lulu” kwa ajili ya kundi hilo. Ofisa biashara wa benki hiyo, Prosper William amesema jukwaa hilo la biashara ni la kwanza kufanyika kwa mwaka 2019 na benki hiyo, ukiachana na mengine yanayotegemea kufanyika katika mikoa mingine.
Kupitia jukwaa hilo, wanawake hao, wamiliki wa biashara ndogo, za kati na kubwa ambao ni wateja na wasio wateja wa benki hiyo wamepata ujuzi kuhusu usimamizi wa biashara zao, ulipaji wa kodi na kuweka mapato yao benki ili kukuza biashara zao. Ofisa huyo ameeleza kuwa lengo la benki hiyo ni kuhakikisha kuwa wanawake wanafundishwa maadili ya biashara na utendaji, pamoja na kusaidiwa kujiwekea akiba kwa kasi kwa ajili ya siku zijazo.
Naye, Jennifer Bashwas wa EIB amesema kuna umuhimu wa kutumia benki kama chombo cha kujipatia mikopo au kuweka akiba ili kufikia malengo binafsi. Mafunzo hayo yamelenga kukuza uongozi mzuri na kazi ya timu katika biashara na maisha binafsi.