Aliyekuwa Spika wa Bunge hapa nchini Anna Makinda ametoa wito kwa wanawake kuondokana na fikra za kuwezeshwa na badala yake amewataka kujiamini na kujiinua kiuchumi akisema wanawake wakiwa waadilifu na wenye nidhamu, basi wanaweza kutwaa madaraka na kuwa viongozi katika Nyanja tofauti hapa nchini na hata kimataifa.
Makinda alitoa wito huo jijini Dar es salaam alipokuwa anawasilisha mada katika tamasha la 14 la jinsia ambalo liliandaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) ambapo alisema wanawake hasa wale walio pembezoni wamekuwa wanyonge kiuchumi kwa muda mrefu sasa huku akiwashauri wajiamini na kuwa mfano katika jamii ikitokea wanapata nafasi ya kuongoza popote pale.
Ameshauri wanawake kutokubali kudhalilishwa, kutumiwa au kushushwa endapo wana elimu, ujuzi na sifa ambazo zinawawezeshwa kufanya kazi yoyote. Amesema ni muda wa wanawake kuacha kujidekeza. Amewashauri kusema kidogo na kusikiliza wanayoambiwa zaidi ili kuelewa jambo na kulifanyia kazi akisema kuzungumza sana hakuna manufaa yoyote.