Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri (ATE) Dk. Aggrey Mlimuka amezishauri taasisi binafsi pamoja na za serikali kuwekeza zaidi kwa wanawake kwa kuwapatia nafasi za juu katika uongozi kwani wamekuwa wakitekeleza majukumu yao vizuri. Dk. Mlimuka amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mkutano mkuu wa mwaka wa wanawake katika uongozi unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba na kusisitiza kuwa endapo taasisi zitawekeza zaidi kwa wanawake, zitapata tija kwani wanazitendea haki nafasi za uongozi wanapozipata.
“Waajiri watambue kuwekeza kwa wanawake watapata faida kubwa. Ukiangalia tija ya ufanyaji kazi ipo chini ikilinganishwa na nje ya nchi, hivyo wakiwekeza katika wanawake, kampuni ama taasisi itasaidia kunufaika”. Ameeleza Mkurugenzi huyo.
Katika maelezo yake Dk. Mlimuka amesema tafiti mbalimbali zimedhibitisha kuwa taasisi nyingi zilizofanikiwa zina wanawake katika nafasi za juu hivyo chama hicho kimejipanga kulifanikisha jambo hilo kwa wanachama na hata wale wasio wanachama ili kuunga mkono harakati za kujenga Tanzania ya viwanda ili kufikia uchumi wa kati inapofika mwaka 2025.