BENKI ya Standard Chartered imetangaza uzinduzi wa program ya Goal ikishirikiana na taasisi ya BRAC Tanzania.
Programu hiyo imelenga kuwawezesha wasichana kupitia michezo na taaluma za maisha.
Programu hiyo imeingia katika awamu yake ya pili.
Kwa mujibu wa Benki ya Standard Chartered program hiyo inawezesha wasichana kujifunza mambo ambayo yatawafanya kuwa viongozi wa kiuchumi katika familia zao, jamii na taifa.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajenga wasichana hao katika ngazi za kujiamini, elimu na ujuzi mahsusi wa kuwafanya kuwa viongozi.
Programu hiyo awali ilizinduliwa nchini Tanzania mwaka 2013 na kulenga kuwafikia wasichana na wavulana 15,000 katika kipindi cha miaka miwili ikiwapatia uwezo wa taaluma za maisha.
Mkuu wa Masuala ya Kisheria, Masoko na Bidhaa wa benki hiyo, Juanita Mramba amesema benki hiyo imefurahishwa na mafanikio katika awamu ya kwanza hasa kutokana na jamii kuwa na msisimuko mkubwa wa program hiyo na hasa wasichana walivyowezeshwa kubadilisha maisha.
Awamu mpya ya programu ya GOAL imelenga kuwapatia taaluma za ujasiriamali na hali ya kuajirika kwa kuzingatia ajenda za kitaifa ya kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Sanjay Rughani alisema ni matarajio yake kwamba wasichana watapatiwa ujuzi unaohitajika ili kuwawezesha kuanzisha na kuendesha biashara zao kuajiri wengine na hata wao kuajiriwa.
Kwa mujibu Juanita, programu hiyo itaambatana na mafunzo ya michezo na elimu. Alisema wale ambao wataonesha uwezo mkubwa wa uongozi wataingizwa kuwa machampioni wa Goal.
Ili kuifanikisha programu kuwa endelevu Goal inaendeshwa kwa mtindo wa kufunza walimu.
Programu hiyo inaendeshwa kwa pamoja kati ya benki hiyo na BRAC Tanzania ambayo ina sifa ya kuwawezesha watu waliokosa nafasi kupata elimu.
BRAC Tanzania pia imejijengea uwezo mkubwa kuwawezesha wasichana kupata taaluma wanazohitaji katika maisha na kuwapatia nafasi ya kupata mikopo midogo na uanzishaji wa viwanda na biashara ndogo.
Chini ya program ya GOAL, BRAC Tanzania itasaidia wasichana kati ya miaka 13-24 kufikia kiwango cha juu cha kiuchumi kwa kuwawezesha mafunzo na kuwapatia usimamizi.
Programu hiyo itahakikisha inawapatia uwezo wa kuanzisha biashara katika Nyanja kama ya ushoni, ususi na kilimo. Programu hiyo pia itawawezesha wasichana kupata kazi kokote.
Rughani amesema kwamba awamu mpya ya GOAL itsaidia kukuza ujasiriamali na utengenezaji wa nafasi za ajira.