Na Mwandishi wetu
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk. Inmi Patterson amesifu jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na Shirika la Vijana Tanzania (TAYOA) katika kusaidia na kuhamasisha vijana ili wajikwamue kiuchumi pamoja na kushiriki katika shughuli za kuleta maendeleo hapa nchini.
Dk. Patterson ameyasema hayo wakati wajumbe watano kutoka Bunge la Congress la Marekani walipotembelea ofisi za shirika hilo. Wabunge hao waliokuwa na familia zao walipata fursa ya kushuhudia shughuli za TAYOA kama vile ujasiriamali, utoaji wa elimu ya Ukimwi bure kwa kupitia simu za bure na miradi mingine ya kuinua vijana.
Balozi huyo ameongezea kuwa wamefurahishwa kuona juhudi zinazofanywa na Shirika la TAYOA kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Mrekani. Amesema Tanzania na Marekani zitaendelea kudumisha mahusiano mazuri waliyonayo na kuahidi kuwa serikali hizo mbili zitaendelea kufanya kazi kwa karibu.