Home BIASHARA Biashara zenye mafanikio huzingatia haya

Biashara zenye mafanikio huzingatia haya

0 comment 76 views

Ni rahisi sana kuanzisha biashara lakini linapokuja suala la kuendesha biashara hiyo na kuiwezesha kufikia malengo na hatimaye kufanikiwa. Wengi bado wamekuwa wakipata wakati mgumu kutokana na kukosa muongozo sahihi wa namna ya kuendesha biashara. Licha ya kuwepo kwa changamoto lukuki katika sekta hii, bado ni rahisi kuwa na biashara yenye mafanikio.

Mfanyabiashara yoyote anatakiwa kuzingatia vitu hivi vitatu vya msingi:

Mpango madhubuti

Ikiwa biashara inakosa muelekeo maalum, ni vigumu kuiendeleza na kuhakikisha inafika mbali licha ya jitihada zinazofanyika. Biashara ambazo zina mafanikio zimekuwa zikizingatia mipango waliyonayo hivyo kuwa na lengo ambalo wanalifanyika kazi. Aidha, unapokuwa na mpango wa biashara, hata wafanyakazi wako wanajua nini wanatakiwa kufanya ili kuifikisha biashara husika mahali bora zaidi. Unapoendesha biashara pasipo kuwa na mpango maalum, ni vigumu kuwa na hamasa ya kutimiza malengo uliyojiwekea na hivyo, inakuwa rahisi zaidi kukata tamaa.

Uwekezaji katika rasilimali watu

Ili biashara ifanikiwe unahitaji watu ambao wanajua wanachofanya na wapo katika mazingira mazuri ya kutekeleza majukumu yao bila vikwazo vyovyote. Kama biashara, ni muhimu kuwekeza katika wafanyakazi wako, Jiulize, kama mfanyakazi ana matatizo nyumbani ataweza kufanya kazi yake kama inavyotakiwa? Ni muhimu kuwekeza katika kuhakikisha mazingira ni mazuri ndani na nje ya biashara kwani kwa kufanya hivyo, unawajenga kuwa watu bora zaidi ambao watasaidia kuijenge biashara yako na kuchochea mafanikio. Ni muhimu kutoa mafunzona kuwa na mazungumzo na wafanyakazi wako ili kuondoa hofu yoyote na kuwafanya wajisikie huru kuzungumza na wewe kila wakati bila uoga.

Mafunzo

Inaelezwa kuwa wafanyakazi wengi zaidi huhitaji mafunzo. Hivyo katika biashara, ni muhimu kutengeneza mazingira ambayo yatawezesha wafanyakazi kujifunza ili waweze kukua na kuwa bora zaidi katika kile wanachofanya. Ukiruhusu hili katika biashara, unatengeneza mfumo ambao unaruhusu watu kujifunza, kuuliza maswali, kutoa maoni yao na kujijenga zaidi.

Mara nyingi watu hufikiria kuwa ili biashara ifanikiwe, kitu cha kwanza kabisa kinachohitajika ni kiasi kikubwa cha fedha kisha badala ya hapo, kila kitu kitaenda sawa. Hii inaweza kuwa na ukweli fulani ndani yake lakini fikiria, kama una kiasi cha milioni 10 na unakosa mpango sahihi wa kuendesha biashara yako utafika mbali? Jibu sahihi ni hapana. Kuna vitu vingine muhimu vya kuzingatia. Unapokuwa na mpango madhubuti, watu ambao wana utayari wa kufanya kazi kwa bidiii pamoja na mafunzo sahihi, basi upo katika nafasi nzuri ya kufanikiwa katika sekta hii ya biashara.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter