Home KILIMO Kilimo cha miti: Utajiri uliojificha

Kilimo cha miti: Utajiri uliojificha

0 comment 277 views

Kufuatia ongezeko kubwa la mahitaji ya mazao ya miti hapa nchini, kilimo cha miti kimeendelea kuja kwa kasi hapa nchini. Licha ya kwamba uwekezaji katika aina hii ya kilimo huchukua muda mrefu (takribani miaka saba hadi kumi baada ya upandaji) kuona faida yake, inaelezwa kuwa utajiri wake ni mkubwa na watanzania wengi zaidi wanatakiwa kuchangamkia kilimo hiki.

Unapoanzisha shamba la miti, ni muhimu kuzingatia mambo ya msingi kama aina ya miti, uchaguzi wa shamba, usafi, uchimbaji mashimo pamoja na upandaji. Unapokuwa makini tangu mwanzo, unakuwa katika nafasi nzuri ya kuhakikisha kuwa miti yako itaota vizuri na kuwa na afya. Tofauti na hapo, ukuaji huwa hafifu na kupelekea hasara kubwa. Maandalizi sahihi ya miti huzalisha miti yenye ubora wa hali ya juu.

Mara baada ya kuchagua aina sahihi ya miti unayotaka, ni muhimu kuzingatia hali ya hewa, viwango vya mwinuko na mteremko pamoja na hali ya hewa. Nyanda za Juu Kusini zina udongo mzuri ambao unafaa kwa ajili ya kilimo cha miti ya aina nyingi ikiwemo mitiki, milingoti na mipaina. Udongo wenye rutuba na uwezo wa kupitisha maji na kuyahifadhi kwa muda mrefu ni sifa kubwa katika ustawi wa miti kutokana na kwamba, miti inahitaji maji na virutubisho kutoka ardhini hivyo ni muhimu sana kuzingatia uwezo wa udongo. Inashauriwa kupanda miti katika maeneo ambayo hupata millimita za ujazo 1,000 au zaidi ya mvua kwa mwaka.

Shamba la miti linaweza kuandaliwa kwa kulimwa na jembe la mkono, trekta au jembe la kukokotwa. Inashauriwa kulima upana wa mita moja katika mstari wa kupanda miti au visahani vya upana wa mita moja. Aidha, nafasi inayopendekezwa kutoka mti hadi mti ni mita 3×3 (hususani kwa mipaina) ili kuiwezesha kutanuka na kukua kwa haraka. Nafasi hii inaruhusu miti kupata mwanga na chakula cha kutosha. Miti ya milingoti inaweza kupandwa nafasi ya mita 2.5×2.5 kwa sababu inahitaji kurefuka zaidi kuliko kutanuka.

Pamoja na hayo, njia za kuzuia moto zinapaswa kutengenezwa kila mwaka mara baada msimu wa mvua kumalizika. Hii ni hatua muhimu kwa kufanya hivyo, unapunguza hatari ya kupata hasara na upotevu wa eneo la uzalishaji. Njia ya moto inaweza kuwa na upana wa mita tano hadi kumi kutoka shamba moja hadi jingine kwa sababu njia hizi hutumika kupitisha magari wakati wa mavuno.

Hapa nchini, mikoa ambayo imejikita zaidi katika kilimo cha miti ni pamoja na Iringa, Njombe, Mbeya na Kagera. Mkoa wa Iringa unaongoza kwa kuwa na misitu mikubwa ambayo imepandwa na serikali, mashirika kutoka nje ya nchi na watu binafsi. Kwa mujibu wa wataalamu wa kilimo, heka moja ya shamba ina uwezo wa kuchukua hadi miti 600 ambapo wastani wa gharama ya mti mmoja uliokomaa ni kati ya Sh. 25,000 hadi Sh. 30,000, hivyo mkulima anaweza kuingiza hadi Sh. 18 milioni katika heka moja pekee ya shamba la miti.

Ikiwa umewekeza katika aina hii ya kilimo, ni muhimu sana kujua soko lako na kulima kulingana na mahitaji yaliyopo. Miti ya mipaina na milingoti inaelezwa kubwa na soko kubwa zaidi ndani na nje ya nchi. Serikali yetu ikiendelea kuunga mkono wakulima hususani katika wakati huu ambao tunaelekea uchumi wa kati, kilimo hiki kinaweza kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo yetu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter