Home BIASHARA Unataka kuwa na website inayovutia wateja?

Unataka kuwa na website inayovutia wateja?

0 comment 124 views

Kadri siku zinavyokwenda wajasiriamali wengi zaidi wanaendelea kuona umuhimu wa tovuti katika biashara zao, ili kuweza kutoa habari zaidi kwa wateja wao na kuweza kutangaza bidhaa au huduma kwa undani zaidi. Ieleweke kuwa mjasiriamali anaweza kutengeneza tovuti bure, au kwa kulipia kila baada ya muda fulani. Hivyo kulingana na ukubwa wa biashara, inashauriwa kutengeneza tovuti itakayokidhi mahitaji ya wateja wako kulingana na bajeti uliyo nayo. Wordpress ni moja ya programu maarufu inayotumiwa  na wengi kutengeneza tovuti na blogu za aina mbalimbali.

Mfanyabiashara anatakiwa kujua kusudi maalum la kufungua tovuti ya biashara yake ili kuweza kuhakikisha mwisho wa siku kusudio hilo linatimia. Hivyo ikiwa unataka kuunda  tovuti ya biashara yako au hata ikiwa tayari unayo, ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo ili kuweza kuhakikisha tovuti hiyo kwa namna moja au nyingine inaleta faida katika biashara yako:

Ni muhimu kuzingatia kuwa tovuti hiyo ni kwaajili ya wateja wako na si kwaajili yako. hivyo hakikisha mteja akifungua tovuti hiyo anafikia matarajio yake kuhusu suluhisho la shida au  hitaji lake la kipekee. Hakikisha katika tovuti hiyo maneno na misemo unayotumia wateja wako wanatumia kuelezea maumivu yao kisha onyesha suluhisho la changamoto husika hii itawavutia wateja wengi zaidi kujifunza katika tovuti hiyo na hata kununua bidhaa au huduma yako baada ya kuridhishwa na suluhisho tajwa.

Kuwa na ofa, hii itawavutia wateja wengi zaidi kuifuatilia tovuti yako si tu kwaajili ya kununua bidhaa au huduma bali hata kujifunza au kupata habari mpya kuhusu tasnia husika au hata biashara hiyo kwa undani zaidi. Hivyo jenga mazoea ya kuweka majarida,  ripoti za bure, au hata ushauri wa bure kuhusu bidhaa au huduma husika na hata masuala yanayohusiana. Hii itakusaidia pia kujua wateja wako wanapendelea masuala gani na ni njia zipi utumie ili kuweza kuwafanya wafuatilie zaidi tovuti yako na hata kununua bidhaa au huduma.

Tambua kuwa tovuti yako ni kama uso wa biashara yako mtandaoni, hivyo hakikisha ni tovuti ya kupendeza, inayoelimisha,na kuwahusisha wateja kufanya majadiliano na hata kueleza mrejesho. Hivyo ifanye iwe ya kitofauti,weka habari,vidokezo,hadithi na masuala mbalimbali yatakayowavutia wateja unaowalenga. Hakikisha ni ya kitaalam, hii itawafanya wateja waone kuwa uko makini na mchakato mzima wa ufanisi wa biashara yako.

Ushuhuda ni muhimu hasa katika ukurasa wa nyumbani (home page) wa tovuti yako hasa katika machapisho unayochapisha, kwani wateja wengi wanaamini sana uzoefu ambao wateja wengine wameupata katika biashara yako kabla ya kufanya maamuzi ya kununua au la. Pia kupitia uthibitisho kutoka kwa watu wengine ni rahisi kwa wateja kujua kama watapata huduma ambayo unakuwa umeahidi.

Mbali na hayo, inashauriwa kurahisisha mchakato wa mawasiliano kupitia tovuti yako ili kuwarahisishia wateja pindi wanapokuwa wanataka kuwasiliana na biashara yako aidha kwa maswali zaidi, kununua bidhaa na masuala mengine. Hivyo hakikisha katika ukurasa wa nyumbani kuna mawasiliano kama namba ya simu, anwani, barua pepe, eneo la biashara nk. Pia hakikisha kuna mtu ambaye atakuwa akiwahudumia wateja kupitia mawasiliano hayo kwa uharaka zaidi ili kuepuka kupoteza wateja.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter