Home FEDHABIMA Chagua bima ya kilimo kwa maendeleo ya kilimo.

Chagua bima ya kilimo kwa maendeleo ya kilimo.

0 comment 128 views

Zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wanategemea kilimo kuendesha maisha yao ya kila siku na kuchangia katika pato la taifa. Serikali imekuwa mstari wa mbele kufanya jitihada zote kuwapa ushirikiano mkubwa wakulima nchini kwa sababu viwanda vinategemea malighafi kutoka kwa wakulima. Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanya mageuzi katika sekta ya kilimo kuelekea Tanzania mpya ya viwanda ili kuhakikisha kasi ya kilimo inakwenda sambamba na ile ya viwanda ili kuwezesha viwanda vilivyopo kufanya kazi bila changamoto ya kukosa malighafi.

Majanga ya aina mbalimbali kama vile magonjwa na ukame huathiri kilimo kwa kiasi kikubwa. Wakulima huwekeza fedha nyingi katika kilimo chao na pale majanga kama haya yanapotokea, wanarudi nyuma sio tu katika kilimo bali kifedha pia. Majanga husababisha upatikanaji wa mazao kupungua kwa mfano mahindi yakiathiriwa na wadudu basi wakulima wa sehemu husika hawatopata chakula na hawatoweza kufanya biashara kwa sababu mahindi hayo hawataweza kuyavuna tena kama ilivyotakiwa, hivyo kuleta njaa na umaskini.

Bima ya kilimo humlinda mkulima katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na majanga yanayotokana na hali ya hewa, magonjwa mbalimbali ya mimea, moto na kadhalika. Licha ya makampuni na benki kadhaa kuanzisha bima za kilimo nchini serikali pia imekuwa ikifikiri kuanzisha bima hiyo kwa bei nafuu ili kuwasaidia hasa wakulima wadogo.

Kuna dhana kuwa, bima ni maalum kwa watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Wengi wao wamejiwekea kuwa bima zinawahusu matajiri, mashirika makubwa au watu walioajiriwa, jambo ambalo si kweli. Kuna muda unaweza kukumbwa na matatizo na kukosa hata senti na hapo ndio umuhimu wa kumiliki bima unapotambulika. Kama janga likitokea na mkulima hakujipanga, bima inaweza kusaidia kutatua tatizo hilo pasipo kutumia fedha za ziada na hivyo shughuli nyingine za kilimo kutoathirika.

Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima nchini (TIRA), ndio shirika linaloshughulika na masuala ya bima hapa nchini. Mwezi Februari mwaka huu. shirika hilo liliandaa semina kwa ajili ya kuongelea bima kwenye sekta ya kilimo na kupitia semina hiyo, wakulima walipewa matumaini kwa sababu serikali ina mpango wa kuanzisha bima ya mazao ili kuwanusuru  na majanga ambayo yamekuwa yakiikumba sekta hiyo mara kwa mara.

Ni muhimu kwa wakulima kuelimishwa vya kutosha kuhusu bima. Aidha, bima hiyo iwe ya gharama nafuu ili waweze kuimudu. Hii itaondoa changamoto ya kuanza upya kila wakati janga likitokea na hivyo maendeleo yatakuwa ya kuridhisha. Wakulima nao wanapaswa kuacha uoga na mazoea na kutambua umuhimu wa bima katika kilimo sio tu kwa ajili ya maendeleo yao bali hata kwa Taifa zima.

Kwa ujumla, sekta ya kilimo inapaswa kupewa kipaumbele zaidi ili kuliepusha taifa kupata janga la njaa na kuwasababishia wananchi kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo. Kilimo kikienda vizuri, uzalishaji utakuwa wa  kuridhisha, malighafi zitatosha na kukidhi mahitaji katika viwanda. Katika bajeti ya serikali, masuala kama bima ya kilimo yanatakiwa kupewa uzito ili kusaidia changamoto kubwa zinazoikumba sekta hii na kuzitafutia suluhisho.  Hii itapelekea sekta ya kilimo kuimarika na sera ya  uchumi wa viwanda kufanikiwa.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter