Home LifestyleTravel Kampuni za utalii zifanye haya kuvutia wateja

Kampuni za utalii zifanye haya kuvutia wateja

0 comment 395 views

Utalii ni moja ya sekta yenye mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania. Kupitia sekta hii watanzania na raia kutoka nje ya nchi wamenufaika kwa kuanzisha biashara mbalimbali zinazohusiana na masuala ya utalii.

Moja ya biashara ambayo inashika kasi ni kuandaa safari kwa ajili ya watalii kwenda kutembelea maeneo mbalimbali nchini.

Kampuni zinazojihusisha na uandaaji wa safari hizi zinatakiwa kuongeza juhudi zaidi hata baada ya kujipatia mafanikio ili kuweza kusonga mbele zaidi kwani kila siku mawakala wapya wanaanzisha biashara hii.

Hizi ni baadhi ya mbinu ambazo kampuni inaweza kutumia ili kupata wateja zaidi na kuongezana kuwahamasisha watalii kutoka maeneo mbalimbali kutumia huduma zao pindi wanapokuja kutembea nchini.

Matangazo

Siku zote biashara huanzishwa baada ya kuona mapungufu yaliyopo katika jamii. Ili kupata mauzo zaidi unatakiwa kuwaonyesha wateja faida za kutumia huduma katika kampuni yako.

Badala ya kutumia muda mwingi kushindana na washindani wako, jikite katika kutoa huduma za kipekee ambazo zitawahamasisha wateja kurudi tena.

Kwa mfano unaweza kuwahamasisha wateja kutoa ushuhuda katika tovuti yako au mitandao ya kijamii ili kuwavutia wateja wapya kwa sababu watu husoma maoni ya watu wengine mtandaoni kabla ya kufanya maamuzi hiyo ushuhuda ni nafasi nzuri ya kushawishi wateja wapya.

Mitandao ya kijamii ni muhimu katika biashara hii

Watalii wengi hutumia mtandao hivyo tumia fursa hiyo kuwasiliana na wateja wako kwa kuweka picha, video, kuuliza maswali katika akaunti yako ili kuwajulisha wateja wako wa zamani na wapya kuhusu huduma zilizopo.

Watalii huhamasika kujaribu vitu vipya kutokana na taarifa zinazowekwa katika mtandao

Watalii hufurahishwa na huduma maalum

Kama kampuni, inatakiwa kujiongeza na kujua ni vitu gani vinaweza kuwavutia wateja wako. Kwa mfano ikiwa unajua watalii hupendelea kutembea na kuona mandhari inayowazunguka, unaweza kuwapa darubini bila kuwatoza fedha.

Hivi ni vitu vidogo lakini mara nyingi maana yake kwao inakuwa kubwa. Ni muhimu kuhakikisha wateja wako hawasahau uzoefu waliopata kwako.

Jitahidi kushirikiana na kampuni zingine za kitalii ikiwa ni pamoja na hoteli, migahawa, sehemu za maonyesho ili kuwarahisishia wateja kupata huduma zote muhimu na kuepuka kuhangaika.

Tengeneza vifurushi vya kuvutia, rahisi kuelewa na katika bei rafiki. Epuka kutoza fedha nyingi kwani inaweza kuwa chanzo cha kukosa wateja.

Kwa mfano unaweza kuweka vifurushi vya bei ya chini ambavyo vinaruhusu marafiki kadhaa kuchangia fedha na kutembelea vivutio kama Serengeti, Zanzibar nk. Hii itawahamasisha wengine wengi kujipanga na kulipia kifurushi hicho.

Kitu kimoja ambacho mawakala wa utalii wanatakiwa kufanyia kazi ni masuala ya bei kati ya watalii wa ndani na nje. Ni rahisi kwa watalii kutoka nje kulipia kiasi chochote lakini kwa upande wa watalii wa ndani, ni watu wachache wapo tayari kutumia gharama kubwa kujionea vivutio vilivyopo.

Inaweza kuwa ni bei ya kawaida, lakini ili kuwahamasisha watalii wa ndani, ni vizuri kwa wahusika kuja na mbinu mpya ambazo zitawashawishi watanzania wengi zaidi kutembelea maeneo hayo.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter