134
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imefanya mkutano na Mabalozi wa Tanzania wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi zilizopo kanda ya Asia na Australia kwa lengo la kuimarisha mikakati thabiti ya utekelezaji wa kuvitangaza vivutio vya utalii wakati wa kipindi hiki ambapo sekta ya utalii duniani imeathirika na janga la Corona.
Mkutano huo uliyofanyika kwa njia ya mtandao uliendeshwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANZANIA TOURIST BOARD, Jaji Thomas Mihayo na kuhudhuriwa na Mabalozi wa Tanzania wa ukanda huo; Mhe. Balozi Dkt. Ramadhani Dau wa Malaysia, Balozi Mbelwa Kairuki wa China, Balozi Baraka Luvanda wa India, Balozi Matilda Masuka wa Korea Kusini, Balozi Hussein Kattanga wa Japan, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australia, Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Caesar Waitara pamoja na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT), Dkt. Abdulla Juma.
Akifungua mkutano huo, Jaji Mihayo aliwasihi Mabalozi hao kutumia hadhi zao za kibalozi katika kuwahamasisha na kuwavutia watu mashuhuri, wanamuziki, wanasiasa na mabalozi wenzao wa nchi wanazofanyia kazi ili waje Tanzania kuvitembelea vivutio vya asili.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na kuratibuwa na TTB, Mkurugenzi Muendeshaji wa TTB, Bi. Devota Mdachi aliwasilisha andiko linaloonesha hali ya utalii wa Tanzania kwa sasa na mikakati iliyoanza kutekelezwa ya kutangaza utalii wa Tanzania katika kipindi hii ambacho nchi nyingi zimefunga mipaka yao.
Aidha, kwa upande wao, Mabalozi pia waliwasilisha mikakati yao na hatimaye mapendekezo jinsi ya kuuza utalii kwenye masoko yao hususan baada ya kipindi cha COVID 19. Mojawapo ya maazimio yaliyojitokeza kwenye mkutano huo ni namna ya kutumia teknologia mpya na mitandao ya kijamii ili kufikisha ujumbe wa kuwavutia watalii. Aidha kwa pamoja walikubaliana kuongeza juhudi madhubuti za kutangaza utalii katika makundi mbalimbali kama vile Jumuiya za Wafanyabiashara na Jumuiya za Kibalozi kwenye masoko ambayo huko nyuma Tanzania ilikua haijitangazi.
Juhudi na mkikakati iliyojadiliwa katika mkutano huu unatarajiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka katika masoko hayo. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha mwaka 2018 Tanzania ilitembelewa na watalii 79,852 kutoka ukanda huo wa Asia na Australasia.
TTB inatarajia kufanya mkutano kama huo na mabalozi wa ukanda wa ulaya hivi karibuni ikawa ni muendelezo wa mikakati ya kujipanga vizuri katika kutangaza utalii wa Tanzania baada ya janga la Corona.